Lema, Nassari wadai watamtoa Muhongo bungeni kwa mabavu

Moshi.Mbunge wa Arusha mjini (Chadema) Godbless Lema amesema atamtoa kwa mabavu bungeni Waziri wa nishati na madini,Profesa Sospetre Muhongo katika kikao kijacho cha Bunge endapo atakuwa hajaondolewa kwenye nafasi hiyo.
Mkakati huo wa Lema umeungwa mkono na Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari ambaye pia amepanga kumtoa bungeni kwa nguvu, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge.
“Keshokutwa nakwenda bungeni kufanya kazi moja tu, nikimkuta Muhongo bungeni ndipo nitafukuzwa ubunge moja kwa moja,” alisema Lema huku akishangiliwa wananchi na kuongeza; “Nikimkuta Muhongo bungeni na Chenge bado ni viongozi mimi nitakwenda kumshika Muhongo nimtoe bungeni kwa sababu Katiba inaruhusu kila raia kukemea uovu.”
Profesa Muhongo na Chenge ni miongoni mwa viongozi ambao Bunge liliazimia wawajibishwe na mamlaka zao kutokana na kashfa ya uchotwaji mamilioni ya fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Hata hivyo, wakati Rais Jakaya Kikwete akilihutubia Taifa, Desemba 22 mwaka jana kupitia wazee wa Dar es Salaam, alitangaza kumweka kiporo Profesa Muhongo kwa siku mbili au tatu, ahadi ambayo haijatekelezwa.
Tayari Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema anayehusishwa na sakata hilo alishatangaza kujiuzulu na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka akifutwa kazi.
Kauli ya Lema
Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika juzi katika Viwanja vya Relini mjini Moshi, Lema alisema Januari 27 mwaka huu ataingia bungeni akiwa na lengo moja tu la kumtoa kwa mabavu, Profesa Muhongo.
“Eti Tibaijuka kapewa tu bilioni moja kaondoka, waziri mwenye dhamana hajavuliwa nyadhifa. Rais Kikwete vipi?” alihoji.
Lema alidai kwamba sakata hilo, katibu binafsi wa Rais ambaye hata hivyo hakumtaja kwa jina, ndiye aliyeandika barua kuruhusu fedha za escrow zitoke lakini hadi sasa yuko salama na hajawajibishwa.
Pia, alihoji sababu za Jaji Werema kutofikishwa mahakamani wakati ndiye aliyefanya makosa katika kutoa ushauri uliozaa sakata la escrow badala yake watu wadogo ndiyo wanashtakiwa.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post