Singida. Madiwani wa CCM wilayani Iramba
wamelaani vikali jaribio la kutaka kuuawa kwa bomu mkurugenzi mtendaji
wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba.
Mkurugenzi huyo, Halima Hanjali Mpita alinusurika
baada ya kitu kilichokuwa kwenye bahasha kulipuka kitandani kwake wakati
akijiandaa kutoka. Bahasha hiyo alipewa na katibu muhtasi wake ikiwa na
kadi ya pongezi iliyopelekwa ofisini kwake na watu wasiojulikana.
Jana, madiwani hao pamoja na kulaani kitendo
hicho, wameomba Polisi kuwasaka na kuwakamata wote waliohusika na njama
hizo na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, katibu wa
madiwani wa CCM ambaye anatoka Kata ya Urughu, Simon Tyosela alisema
umoja wao ulitoa tamko hilo kwenye kikao kilichofanyika Alhamisi
iliyopita.
“Kwa ujumla sisi madiwani wa CCM tupo pamoja na
mkurugenzi wetu Halima Mpita na vilevile watendaji wote. Kwa umoja huo
sote kwa pamoja tutaendeleza gurudumu la maendeleo ya wilaya ya Iramba,”
alisema.
Aidha, Tyosela ameiomba polisi pamoja na kufanya
uchunguzi wa jaribio hilo, ichunguze kwa kina ujumbe aliopewa mkurugenzi
huyo kwamba amedhulumu Sh90 milioni kutokana na ‘dili’ walilofanya
pamoja ili ukweli ufahamike.
Katibu huyo alisema wananchi wanataka kufahamu kwa kina suala hilo.
na hatua za kisheria zitakazochukuliwa dhidi ya
watuhumiwa watakaokamatwa kuhusika na jaribio hilo na juu ya ‘dili’ la
shilingi 90 milioni.
Katika hatua nyingine,Tyosela alisema madiwani wa
chama tawala hawafurahishii wala hawapendezwi na msuguano uliopo kwenye
halmashauri hiyo wa watendaji kwa watendaji na watendaji na mkurugenzi
wao.
“Kuna uvumi kwamba baadhi ya watendaji wanataka
kuomba kuhama kwa madai kwamba sisi madiwani hatuwapendi.Hapana sisi
tunawapenda sana watendaji wetu na hatupo radhi kuona mtendaji ye yote
anahama kutokana na misuguano ya ndani kwa ndani ambayo haina tija kwa
wananchi wa wilaya ya Iramba.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment