Majimbo sita ya ubunge ‘yako wazi’


Dar es Salaam. Ikiwa imesalia miezi kumi kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, hadi sasa majimbo sita yako wazi baada ya wabunge wanaoyaongoza kutangaza kutogombea tena ubunge.

Ni wazi kuwa uamuzi wa wabunge hao, wengi wao wakiwa wameamua kupumzika baada ya kushikilia viti hivyo kwa vipindi zaidi ya viwili, utaibua ‘vita kali’, vikianzia ndani ya vyama wakati wa kura za maoni na baadaye baina ya vyama wakati wa kuomba ridhaa kwa wananchi.

Mbunge aliyetangaza kuachia jimbo hivi karibuni ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye amekuwa mbunge wa Katavi kwa vipindi vitatu kuanzia mwaka 2000 akisema anakwenda kufanya kitu kingine.

“Wapo ambao hawatagombea sababu wanataka kuwania urais. Wapo waliotangaza kutogombea sababu tu ya demokrasia na kutaka kuwapisha wengine. Hilo ni jambo zuri,” alisema Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Gaudence Mpangala.

Profesa Mpangala alikumbushia pendekezo lililokuwapo katika Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilipendekeza kuwa mwisho wa kugombea uwe vipindi vitatu.

“Pendekezo lile lilikuwa zuri ili kuwaondoa wanaokaa madarakani zaidi ya miaka 50, ila wapo wanaotangaza kutogombea kwa sababu tu za kisiasa,” alisema.

Vyama vya upinzani pia safari hii vitakuwa na kazi ngumu ya kuteua wagombea baada ya kufikia makubaliano chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kusimamisha mgombea mmoja kutoka miongoni mwao katika ngazi zote kuanzia Serikali za Mitaa.

Vyama vilivyo chini ya mwavuli huo ni NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD, wakati chama kipya cha ACT - Tanzania kilionyesha nguvu katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa na kama hakitamaliza mgogoro, kinaweza kuwa tishio wakati wa kutafuta kura za wananchi utakapowadia.

Bernard Membe (Mtama)

“Unajua nimekuwa mbunge wenu kwa vipindi vitatu. Hivi leo ninawaaga rasmi kuwa sitagombea tena nafasi hii ya ubunge,” alisema Membe katika hafla ya Mwaka Mpya aliyoandaa nyumbani kwake Januari, 2013.

Membe ni miongoni mwa makada wa CCM wanaotajwa kutaka kuwania urais, ingawa amekuwa akieleza kuwa anasubiri “kuoteshwa”. Iwapo atajitosa kugombea kuwania nafasi hiyo ya juu nchini, jimbo hilo litabaki wazi na tayari linawaniwa na kiongozi mmoja wa juu wa CCM.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post