Mambo ya kuzingatia katika mkataba wa ajira

Kama ilivyo kwa mikataba mingine, uhalali wa mkataba ni lazima ujengwe katika nguzo kuu tano ambazo ni makubaliano, hiari ya kuingia mkataba, malipo halali, uwezo wa kuingia mkataba pamoja na uhalali wa shughuli yenyewe itakayofanyika.
Kama ilivyo kwa mikataba mingine, uhalali wa mkataba ni lazima ujengwe katika nguzo kuu tano ambazo ni makubaliano, hiari ya kuingia mkataba, malipo halali, uwezo wa kuingia mkataba pamoja na uhalali wa shughuli yenyewe itakayofanyika.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Sheria ya ajira na uhusiano kazini ya mwaka 2004, mkataba wa ajira ni lazima uonyeshe jina na anwani ya mwajiri na mwajiriwa, tarehe mliyosaini mkataba, tarehe mkataba unapoanza na tarehe mkataba utakapomalizika endapo mkataba huo ni wa muda maalumu.
Mkataba wa ajira pia ni muhimu useme mwajiriwa anaajiriwa katika nafasi gani na ikiwezekana utaje majukumu yake kama mwajiriwa pamoja na mahali atakapofanyia kazi. Itafaa pia kama kipengele cha namna ya kusitisha mkataba kitakuwepo endapo upande wowote utahitaji kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria.
Mkataba wa ajira ni lazima uweke wazi haki na wajibu wa mwajiriwa kwa mujibu wa sheria za kazi. Mambo hayo yanaweza pia kuorodheshwa kwenye sera ya kazi ya mwajiri endapo atakuwa nayo. Haki za mwajiriwa ni pamoja na; kiwango cha mshahara stahiki, likizo na siku za mapumziko, saa za kazi, malipo ya asilimia kumi (10%) za mfuko wa hifadhi ya jamii kutoka kwa mwajiri, malipo ya muda wa kazi wa ziada (overtime), haki ya kujiunga na chama cha wafanyakazi na mambo mengine muhimu.
Wajibu wa mwajiriwa hujumuisha kufanya kazi kwa bidii, usiri, kutunza muda, nidhamu, kutimiza na kufikia malengo ya mwajiri, kulipa kodi, kujiunga na mfuko wa hifadhi ya jamii na mengineyo kwa mujibu wa sheria.
Haki na wajibu wa mwajiri ni muhimu pia ukaelezwa katika mkataba wa ajira.
Kimsingi haki za mwajiriwa kwa upande mmoja ni wajibu wa mwajiri kwa upande mwingine na wajibu wa mwajiriwa kwa upande mmoja pia huwa ni haki za mwajiri kwa upande mwingine.
Hivyo kila upande ukitimiza wajibu wake, kila upande utapata haki zake pasipo kikwazo chochote.
Ikumbukwe kwamba, ni kosa kisheria kumwajiri mtu pasipo mkataba wa ajira. Pia ni kosa kisheria kumwajiri mtoto wa chini ya umri wa miaka 14. Kwa mujibu wa kifungu cha 5 cha sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004 mtoto wa umri wa miaka 14 hadi 17 anaweza kuajiriwa kwa kazi nyepesi na ambazo hazitamdhuru kiafya wala kuathiri mahudhurio na maendeleo yake shuleni.
Mkataba wa ajira hulinda mustakabali wa ajira, huondoa migogoro isiyo na lazima na huweka uwazi na uwajibikaji wa pande zote mbili.
Usikubali kuajiriwa au kuajiri pasipo mkataba. Ikiwezekana mtafute wakili/mwanasheria akusaidie kuandika na kupitia mikataba yako. Hakikisha una mkataba wa maandishi wa ajira yako. Pande zote mbili zinapaswa kuwa na nakala ya mkataba huo.

Post a Comment

Previous Post Next Post