‘Matumizi makubwa ya fedha vyama vya siasa yanatia shaka’

Wataalamu wa kilimo huwashauri wakulima kuchagua mbegu bora za kupanda kwenye udongo mzuri ulio na rutuba, ili zizae na kuleta mavuno yenye faida.
Nao wanasiasa wanautazama mwaka huu 2015 wa Uchaguzi Mkuu kama shamba lililo na rutuba, lakini mkulima hana uhakika na mbegu alizoshika mkononi kwamba ni ipi itampa matokeo mazuri.
Ni ukweli usiofichika kwamba kwenye miaka ya karibuni, vyama vya siasa vimekuwa vikitumia fedha nyingi kwenye mikutano yao na ndani na nje, ili kuhakikisha kuwa mtu anayechaguliwa na chama anakibeba kwa kuzaa matunda mema ya kupata madaraka, jambo ambalo linatia shaka.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti uitwao ‘Upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ushindani wa kisiasa’, Profesa Mohabe Nyirabu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema ongezeko la matumizi makubwa ya fedha kwenye vyama vya siasa linatia shaka.
Anasema kuwa kwa jumla vyama vya siasa vipo katika wakati mgumu ‘vikihaha’ kutafuta fedha nyingi za kufanyia kampeni na kutafuta wanachama wapya, lakini huku vikipoteza imani yao mbele ya wananchi kuhusu matumizi ya fedha.
Profesa Nyirabu anasema kuwa matumizi ya fedha nyingi kwenye vyama vya siasa yameongezeka zaidi baada ya kuanzishwa kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.
“Kama matumizi ya fedha nyingi na utoaji wa rushwa umekithiri katika jamii, zinatakiwa sera zinazosimamia matumizi ya fedha ndani ya vyama hivyo ziboreshwe,” anaeleza Profesa Nyirabu.
Msomi huyo kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Uongozi wa Umma ya Udsm, anasema katika nchi yenye mfumo wa kidemokrasia, umma huvichangia fedha vyama kwa sababu kuu tatu.
Sababu ya kwanza ni kwa ajili ya kuviwezesha vyama hivyo kukua na kusambaza itikadi na sera zake kwa wanachama wake. Pia, michango ya fedha hukipa chama uhakika wa kuendelea kuwapo na kukinusuru na ushawishishi kukisambaratisha. Anataja lengo la tatu la michango hiyo kwa vyama vya siasa kuwa ni kuviwezesha kusimama kidete dhidi ya ushawishi kutoka taasisi binafsi na mashirika ya kigeni.
Profesa huyo anasema kwamba kwa kuwa baadhi ya vyama vya siasa vinaonekana kutumia fedha nyingi kuliko mapato yanayopatikana, kuna haja ya vyanzo vya mapato hayo kuwekwa bayana.
“Kuwa na mapato kwenye vyama vya siasa siyo jambo baya, matokeo ya mara kwa mara ya rushwa kwenye uchaguzi ni dalili za kuwapo kwa tatizo linalohusu matumizi ya fedha nyingi kwenye siasa,” anasema Profesa Nyirabu.
Matokeo ya utafiti huo yanaeleza kuwa wakati wa mfumo wa chama kimoja cha siasa, mapato kwa ajili ya kuendesha chama hicho yalitokana na michango kutoka kwa wanachama

Post a Comment

Previous Post Next Post