Mawaziri wa escrow hawatuhusu-Hoseah

Dar es Salaam. Wakati wananchi wakisubiri vigogo wa serikalini na mawaziri wanaotuhumiwa kuhusika kwenye kashfa ya uchotaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow kufikishwa mbele ya vyombo vya umma, ni watumishi watano tu wa umma waliofikishwa mahakamani, lakini Mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hoseah ana jibu la suala hilo; kazi yao ni kufikisha mahakamani ‘vidagaa’.
Katika kashfa hiyo ya Sh306 bilioni, mawaziri wa sasa na zamani pamoja na makatibu wakuu wa wizara, wanatuhumiwa kwa njia moja au nyingine kuhusika kwenye kufanikisha kwa makusudi au uzembe uchotwaji wa fedha hizo, kuikosesha mapato Serikali na kupokea mgawo wa fedha hizo, lakini hadi sasa ni watumishi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Tanesco na Benki Kuu (BoT) pekee waliofikishwa mahakamani.
Wote watano, ambao ni vigogo kwenye taasisi zao, wameshtakiwa kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ili kufanikisha mkakati huo ulioibuliwa na gazeti la The Citizen na baadaye Bunge kulidaka na kufikia maazimio ya kutaka wahusika wote wawajibishwe na mamlaka zinazowahusu.
Juzi, mkurugenzi huyo wa Takukuru aliliambia gazeti hili kuwa taasisi yake itaendelea kuchunguza watu wote waliohusika katika kashfa ya escrow bila ya ubaguzi, lakini akabainisha kuwa kazi ya kuwapeleka mahakamani mawaziri na vigogo inatakiwa ifanywe na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Dk Hoseah, ambaye aliwahi kuingia kwenye mzozo wa DPP wa zamani kutokana na madai yake kuwa mafaili mengi ya kesi za rushwa hayafanyiwi kazi, alisema sheria haiwaruhusu kuwapeleka mahakamani mawaziri iwapo watabainika kuhusika kwenye vitendo vya rushwa.
Kwa mujibu wa kifungu cha 57 cha Sheria Namba 11 ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Mwaka 2007, endapo vigogo na mawaziri watabainika kuhusishwa na vitendo vya rushwa, jalada la uchunguzi wao litakabidhiwa kwa DPP ili achukue hatua ya kuwapeleka mahakamani.
Dk Hoseah alisema kwa sasa Takukuru inaendelea na uchunguzi wake mpaka itakapojihakikishia ushahidi wa kutosha dhidi ya vigogo hao.
“Bunge lilitoa maazimio yake na likaagiza kuchukuliwa hatua…Takukuru tulishaanza na tunaendelea na uchunguzi. Taratibu zote zikishakamilika kisha ushahidi ukapatikana kwa vielelezo vyote, basi watafikishwa mahakamani wala hakuna tatizo lolote,” alisema.
“Lakini watafikishwa mahakamani baada ya sisi kuwasilisha jalada letu la uchunguzi kwa DPP ambaye ndiye mamlaka ya kuwafikisha mahakamani kama sheria inavyotuagiza.”
Udhaifu huo wa sheria pia ulizungumziwa na Bunge wakati wa kujadili kashfa ya escrow na kuazimia kuwa sheria inayounda Takukuru ifanyiwe kazi ili iwe na mamlaka hayo ya kufikisha mahakamani vigogo wa rushwa kubwa.
Waliohusishwa na rushwa
Mawaziri waliotajwa kwenye sakata hilo ni Profesa Anna Tibaijuka, ambaye alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na ambaye aliingiziwa Sh1.6 bilioni na mwanahisa wa zamani wa Kampuni ya IPTL, James Rugemarila. Tibaijuka alivuliwa wadhifa huo kutokana na sakata hilo
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post