Mifumo ya Kopunovic ni baab kubwa


Kocha wa Simba, (kulia) Goran Kopunovic.
Sweetbert Lukonge na Kazija Thabit, Zanzibar
SIMBA inatarajiwa kushuka uwanjani kukipiga dhidi ya JKU katika nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi, leo Jumamosi, lakini tayari Kocha wa Simba, Goran Kopunovic, ameonyesha kujiamini na kutoa mafunzo makali kwa wachezaji wake.

Kocha huyo raia wa Serbia, jana alitumia dakika 60 kukiandaa kikosi chake kwa ajili ya mechi hiyo ambapo alionekana kutumia muda mwingi kutoa maelekezo ya kushambulia na kuzuia kwa wachezaji wachache.
Ilikuwa hivi:  Kopunovic aliwasili mapema, majira ya saa kumi jioni kwenye Uwanja wa Amaan na kuanza kuzunguka uwanjani hapo mwenyewe, huku akionekana kutafakari mambo kadhaa.Muda mfupi baadaye wachezaji wake waliwasili na moja kwa moja wakaanza mazoezi mepesi pamoja, lakini baada ya muda akawagawa makundi mawili, moja akawa analisimamia yeye, lingine likiwa chini ya msaidizi wake, Selemani Matola.
Wachezaji ambao aliwasimamia yeye ni mabeki Rajabu Isihaka, Juuko Murushid, kisha kuwataka kuwazuia Simon Sserunkuma, Ibrahim Ajibu, Dan Sserunkuma na Elias Maguli.Makipa wa Simba, wakiongozwa na Ivo Mapunda ambaye alianza mazoezi jana baada ya kukosekana kwa muda, walikuwa na kazi kubwa ya kuzuia washambuliaji hao katika mfumo huo uliokuwa ukitumiwa na kocha wao.
Ilikuwa kazi ngumu kwa mabeki hao wa Simba lakini mpaka mazoezi yanakamilika, kocha huyo alionekana kuridhika kwa kile alichokitaka.Kocha huyo ambaye ameiongoza Simba katika mechi mbili na zote akiibuka na ushindi, alipofuatwa na gazeti hili baada ya mazoezi alisema kuwa anawahi kwa kuwa alikuwa na mazungumzo na wachezaji wake usiku wa jana bila kufafanua ni mazungumzo ya nini.

Post a Comment

Previous Post Next Post