Dar es Salaam. Licha ya Bunge kuazimia kuwa
wenyeviti wa kamati zake waliotajwa kuhusika kwenye kashfa ya Akaunti ya
Tegeta Escrow wavuliwe nyadhifa zao, hali imekuwa tofauti katika vikao
vya kamati hizo vilivyoanza jana baada ya baadhi yao kuongoza vikao
hivyo. Jana, Kamati Kuu ya CCM imeamua viongozi hao, Andrew Chenge,
William Ngeleja Na Profesa Anna Tibaijuka wafikishwe Kamati ya Maadili
ya chama.
Awali, walitakiwa kuachia ngazi na kamati zao
katika mabano ni Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala), Chenge (Bajeti) na
Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini).
Kikao cha 16 na 17 cha Bunge kiliazimia kuwa
kamati husika za kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka na kwa
vyovyote vile kabla ya Mkutano wa 18 wa Bunge unaoanza Januari 27,
kuwavua nyadhifa zao wenyeviti tajwa wa kamati husika.
Hata hivyo, jana, Ngeleja alisema anaendelea na madaraka yake, kwa kuwa hatua iliyopo sasa ni ya uchunguzi.
“Mimi naendelea na kazi zangu kama mwenyekiti wa
kamati, najua uchunguzi wa suala hili bado unaendelea, baada ya hapo
ikithibitika ndipo Bunge litachukua uamuzi nami sitakuwa na budi
kutekeleza,” alisema Ngeleja.
Aliongeza: “Ingawa ninajua kuna shinikizo kwa baadhi ya watu kwa sababu wanazozijua wao hawapendi kutuona katika nafasi hizi.”
Kwa upande wake, Chenge alisema: “Sikuwahi
kutangaza kujiondoa katika nafasi hii ya uenyekiti. Nimeshangaa taarifa
zilizotolewa katika baadhi ya vyombo vya habari.”
Alisema tuhuma zinazomkabili hazimuumizi kichwa
kwa sababu hazina ukweli, “Dhamira hainiumi kwa sababu siwezi kushiriki
kuiba fedha za wananchi. Mimi ni kama tumbili hata hapa nitaruka.”
Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Festus Limbu
alisema suala la Chenge linasubiri uamuzi utakaotolewa na Spika wa
Bunge, Anne Makinda. “Kamati imeamua kwa busara Chenge akae pembeni na
makamu mwenyekiti aongoze vikao huku ikisubiri hatua atakazozichukua
Spika (Makinda)...lakini siyo taarifa kwamba Chenge kajiuzulu, siyo
kweli.”
“Unajua suala hili unaweza kusema bado ni bichi,
Chenge ni mwenyekiti mteule wa Spika, lakini wenyeviti wengine
wanachaguliwa na wajumbe wa kamati zao, labda Spika hajaona wa kumteua
au anataka kuiachia kamati ifanye uchaguzi, hili litategemea na yeye,”
alisema Limbu ambaye ni Mbunge wa Magu (CCM)
Kuhusu wafadhili wa maendeleo ambao kamati hiyo
ilikutana nao jana alisema wametoa asilimia 50 ya Dola 558 milioni
ambazo wahisani hao waliahidi.
Kikao cha Kamati ya Nishati na Madini kiliongozwa
na Makamu mwenyekiti wake, Jerome Bwanausi ambaye alilithibitishia
gazeti hili kwamba hawakufanya uchaguzi wowote.
- MWANANCHI
- MWANANCHI
Post a Comment