Panya Road wana nguvu kuliko Dola?

Katuni.
Kuna taarifa kuwa Jeshi la Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam linaendelea vyema na msako mkali wa kuwanasa vijana wanaotuhumiwa kuwa miongoni mwa wanachama wa kundi la uhalifu la 'Panya Road'.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Kanda hiyo, hadi kufikia mwishoni mwa wiki tayari kulikuwa na watuhumiwa 36 waliotiwa mbaroni na kufikia jana jioni, idadi yao iliongezeka baada ya wengine 510 pamoja na viongozi wao kadhaa kudaiwa kupatikana.

Kundi hilo lilitajwa kuhusika katika vitendo vya uhalifu vilivyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye mitaa kadhaa ya jijini Dar es Salaam na kuwasababishia madhara wananchi huku wengine wakipata usumbufu mkubwa kutokana na hofu iliyosambaa karibu katika kila kona ya jiji.

Kundi hilo lenye kawaida ya kutumia silaha za kienyeji kama nondo, mikuki, mapanga,  fimbo, visu na mawe, lilikatiza kwenye baadhi ya mitaa na kushambulia watu, kuwajeruhi na kisha kufanikiwa kuwapora mali zao.

Awali, baadhi ya makamanda wa Polisi jijini Dar es Salaam walikana juu ya kuwapo kwa Panya Road. Wakasisitiza kuwa huo ulikuwa ni uvumi tu.

Hata hivyo, baadaye Polisi waliibuka na kauli nyingine kuhusiana na Panya Road, wakikiri juu ya kuwapo kwa kundi hilo na kueleza kwamba chanzo juu ya kile kilichotokea ni madai kwamba mmoja wa wanachama wao (Panya Road) alituhumiwa kuhusika katika tukio la wizi na kuuawa na wananchi wenye hasira katika siku ya mkesha wa mwaka mpya.

Ilielezwa kwamba kufuatia matukio hayo ya Panya Road, Polisi waliwakamata watuhumiwa 36 wenye umri kuanzia miaka 16 hadi 30. Na jana ndipo ikatolewa taarifa ya kukamatwa kwa watuhumiwa wengine zaidi ya 500.

Hakika, kuna simulizi nyingi kuhusiana na uwapo wa 'Panya Road'.  Mengine ni ya kweli na mengine huongezwa chumvi na baadhi ya watu katika namna ambayo kwa bahati mbaya huwasababishia hofu zaidi wananchi.

Jambo moja muhimu kwa jeshi la polisi ni kuzingatia upokeaji wake taarifa kuhusiana na matukio ya kihalifu na namna ya kutoa mwitikio kwa umma.

Tukio hili la Panya Road limedhihirisha kuwapo kwa kasoro kubwa katika eneo hili. Kwa mfano, wapo wananchi walioripotiwa wakilalamika kuwa licha ya kutoa taarifa mapema kwa jeshi la polisi kuhusiana na uwapo wa Panya Road katika maeneo yao siku ya tukio, hakuna walichokiambulia bali kukatishwa tamaa. Kwa mfano, wapo walioambiwa kwamba huo ni uvumi tu.

Kama hiyo haitoshi, Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam akakaririwa akisema vilevile kuwa hakuna ukweli wowote juu ya Panya Road. Kwa kiasi fulani, taarifa hizi kutoka polisi ziliwachanganya wananchi kwani ukweli ni kuwa Panya Road walishapita katika baadhi ya maeneo yao na kuwaachia vilio.

Na hisia kwamba kauli za awali za polisi hazina ukweli zilijidhihiri baada ya jeshi hilo kukiri kuwa Panya Road walifanya uhalifu.

Licha ya kufahamu kwamba Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam walishatoa ufafanuzi zaidi jana kuhusiana na suala hilo, sisi bado tunadhani kwamba ipo haja kwa jeshi la polisi kujiangalia upya katika eneo hili la upokeaji taarifa za matukio ya kihalifu kutoka kwa wananchi, kuzifanyia kazi taarifa hizo na kisha kutoa ufafanuzi kwa umma katika namna isiyokuwa na shaka.

Isitoshe, kuna umuhimu pia wa jeshi hilo kushirikiana zaidi na wananchi ili kuhakikisha kwamba uchunguzi zaidi unafanyika na wahusika wote wanafikishwa mbele ya mkono wa sheria.

Kwamba, ni vizuri jeshi la polisi likatumia vyema rasilimali kubwa ya vifaa na watu makini na weledi walio nao katika kudhibiti uhalifu. Kamwe wasikubali wananchi wasumbuliwe na vikundi vya namna ya Panya Road. Ni imani yetu kwamba katika muda mfupi ujao, kikundi hiki kitabaki kuwa historia jijini Dar es Salaam kama ilivyokuwa 'Kiboko Msheli', 'Comandoo Yosso' na 'Mbwa Mwitu'.

Ni imani yetu kuwa Panya Road watasakwa kwa udi na uvumba na kupelekwa kwenye mkono wa sheria kwani daima, nguvu za Dola haziwezi kuchezewa na wahuni wachache wanaowakosesha amani wananchi kwa mikuki, nondo, visu, mawe na pengine jeuri itokanayo na matumizi ya dawa za kulevya.

 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post