Sakata la Escrow, Mwigulu atoa siku 30 walionufaika walipe kodi

*Ataka watendaji walioiibia Serikali watupwe rumande
Nyendo Mohamed na Suleiman Msuya
NAIBU Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba ametoa siku 30 kwa watu waliopata fedha za akaunti ya Tegeta Escrow kukamilisha mchanganuo uliopelekwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Amesema kitendo cha viongozi na watendaji ambao wanaiibia Serikali na kusababisha wakwepaji kodi kuachwa wakiendelea kuwepo mitaani, ni sawa na kuwafanyia hafla ya kuagwa (Sendoff), baada ya kufanya maovu.
Pia, alisema kama Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), chama chao hakitakuwa genge la majambazi, hivyo lazima hatua zichukuliwe na kodi ilipwe.
Hayo aliyasema jana Dar es Salaam katika mahojiano kwenye kipindi cha Power Breakfast cha Clouds Fm, kuhusiana na utekelezaji wa maagizo mbalimbali katika sakata la Escrow.
Nchemba alisema kwa siku za hivi karibuni kumeibuka watu wenye nyadhifa mbalimbali ambao huisababishia Serikali hasara kwa kuiba au kuruhusu kodi ikwepwe, matokeo yake hujiuzulu au kusimamishwa, jambo ambalo husababisha waende kutumia fedha hizo.
Alisema angefurahi kama wahusika wote wa kashfa za wizi, ufisadi, rushwa na kulipotezea taifa kodi, wakapelekwa mahabusu, huku kesi zikiendelea ili iwe fundisho kwa wengine.
“Naona sasa imekuwa kama kamtindo kwa baadhi ya watu wanaiba, wanasababishia hasara  kwa nchi, halafu wanasimamishwa kazi wanaendelea kula maisha mitaani, naona kama vile wanafanyiwa ‘sendoff ‘  jambo ambalo halikubaliki,” alisema Nchemba.
Alisema kutokana na tabia hiyo kuendelea, jamii inaonekana kukosa imani na viongozi na watendaji ambao wanawawakilisha katika maamuzi mbalimbali.
Naibu Waziri huyo akizungumzia suala ukwepaji kodi, hasa za mgao wa Escrow, alisema lazima ilipwe na tayari waliopokea fedha hizo wamepelekewa mchanganuo wa kodi, ambapo wamepewa siku 30 kukamiliasha mchanganuo huo na kuupeleka TRA.
“Utaratibu wa kikodi hata kwenye biashara za kawaida, TRA huwa wanapeleka hesabu zake na wewe mwenye biashara yako unachotakiwa kufanya ni kumtumia mhasibu wako aseme, maana kodi unalipa katika faida, hivyo aseme kipato kilikuwa kiasi gani na ulitumia gharama gani kupata kipato. Kama kuna ghala utoe katika faida ili ulipe kodi.
“Hivyo, alisema ni lazima kodi inayostahili ilipwe, kwani hatuwezi kukimbizana na mama mjane au mtoto yatima anayeuza mchicha kwenye makapu na kuacha kodi kubwa kiasi hicho,” alisema
Alisema kuwa, hadi sasa kuna maofisa saba wa TRA wamesimamishwa kazi ili kutimiza taratibu za kiutumishi katika kuwashughulikia, kwasababu mtu aliyesoma kwa kodi za Watanzania na kuaminiwa kukusanya kodi, badala ya kuandika dola milioni 6, akaandika fedha za Tanzania sh. milioni sita, mtu huyo hana sehemu ya kuponea.
Bajeti
Kuhusu bajeti, alisema kusitishwa kwa misaada kwa wafadhili, wametumia fedha za ndani kwa kiasi kikubwa zaidi ya sh. bilioni 200 kwenda kwenye miradi ya maendeleo, kama barabara, maji na umeme na elimu ya hali ya juu.
Mwigulu alikiri kuwa, ni kweli wahisani walisitisha misaada, lakini habari njema ni kwamba, baada ya kusomwa kwa taarifa bungeni, wafadhili waliandika barua kuwa, wameridhika na ameona hatua zilizochukuliwa na Serikali, tayari walianza kutoa fedha.
Nchemba alisema katika hilo, Serikali inatakiwa kujifunza kuwa, sasa kama taifa wanatakiwa kujitegemea kwani kupaga mipango ya maendelo na kutegemea nchi nyingine kutoa gharama wanapopenda, ni tatizo kubwa na inatokea kwasababu wamekuwa tegemezi.
Aliongeza kuwa, kama wanataka kujitegemea na kutoka katika hili, hatua ambazo zinachukuliwa na Serikali zinatakiwa kuungwa mkono, lakini kuwa na uadilifu katika matumizi ya fedha na si za wahisani tu, na kodi za Watanzania.
Kupanda kwa mafuta
Alisema kilichosababisha kutoshuka kwa mafuta inatokana na kutokuwepo kwa uzalendo, kwa wafanyakazi na wafanyabiashara.
“Inatakiwa kama taifa kuliangalia hili, taasisi inayopanga bei Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati, Maji na Mafuta (Ewura), na wenyewe wanaishi kwa bei hiyo ya mafuta.
“Bei ikiwa kubwa, kipatao chao kinaongezeka, hivyo inahitaji unazelndo wa hali ya juu kwani wanaposhinikiza bei kushuka na kipato chao kinashuka,” alisema.
Hivyo, alisema katika suala hilo kuna mgongano wa kimaslahi katika taasisi yenyewe ya kusimamia na wafanyabishara, katika usimamizi unaposimamia na kukusanya mwenyewe, huku usimamizi wao ukitegemea hicho hicho, ni hatari.
Alisema katika hilo, linatakiwa kutenganisha kuwepo kwa wanaosimamia na wanaofanya utekezaji mwingine.
Mishahara hewa
Naibu Waziri huyo wa Fedha, alisema kumekuwa na ulipaji mishahara hewa, lakini yao inapambana na hali hiyo ili fedha hizo zibainishwe, ambapo kila tarehe 10 mwahiri anatakiwa kuwasilisha orodha ya wafanyakazi wanaostahili kulipwa.
Alisema kuwa, hawawezi kulia kila siku kuwepo kwa mishahara hewa, hivyo wanatakiwa kujua kuwa, ni vitendo visvyofaa.
“Kuna maofisa utumishi ambao hulipwa kutokana na kodi za Watanzania, hili wanatakiwa kulifanyia kazi kuhakikisha wanaofanya hivyo wanachukuliwa hatua za kisheria,” alisema.
Kuhusu kuwania urais
Nchemba alisema kuwa, wakati ukifika atasema, lakini kwa sasa amepewa nafasi ya kusaidiana na Waziri wa Fedha, hivyo analikamilisha hilo kwanza kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi.
”Nilipokea taarifa mbalimbali kutoka kwa vijana, viongozi wa dini, wazee na hata vijiweni wakinitaka nigombee urais, lakini kwa sasa acha nimalize haya majukumu niliyonayo,” alisema.
Mwambalaswa
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini ambaye pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Victor Mwambalaswa amesema hawezi kujiuzulu mpaka akutane na wajumbe wa kamati yake jijini Dar es Salaam.
Aidha, alisema hawezi kujiuzulu akiwa jimboni kwake, kwani kanuni za Bunge hazimtaki afanye hivyo.
Mwambalaswa aliyasema hayo jana, ikiwa ni siku chache baada ya taarifa kutoka katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti ya Bunge, Andrew Chenge amejiuzulu nafasi hiyo, ikiwa ni utekelezaji wa azimio la Bunge ambalo lilitaka wenyeviti hao kuwajibishwa.
Alisema suala la kujiuzulu ni la kawaida, lakini hawezi kufanya hivyo akiwa jimboni kwa kile alichodai kuwa, kanuni za Bunge hazimwelekezi afanye uamuzi huo.
“Siwezi kujiuzulu nikiwa jimboni mpaka nikutane na wajumbe wa kamati yangu, kwani ndivyo kanuni zinavyotaka kinyume na hapo siwezi kufanya uamuzi huo,” alisema Mwambalaswa.
Jambo Leo ilivyoendelea kumng’ang’ania kwanini hafanyi uamuzi huo alijibu kuwa hawezi na akakata simu.
Suala la kujiuzulu wenyeviti hao wa kamati tatu za Kudumu za Bunge la Tanzania, liliibuliwa na taarifa ya Sakata la Akaunti ya Escrow, ambapo Mwambalaswa alihusishwa kupitia nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Wakati Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria, William Ngeleja, Andrew Chenge wakihusika kwa kupata mgao wa fedha hizo kutoka kwa mfanyabiashara James Rugemalila kupitia Benki ya Mkombozi.
Awali, Naibu Spika wa Bunge la Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai alivyoozungumza na Jambo Leo, mwishoni mwa mwaka jana, aliweka bayana kuwa, wenyeviti hao lazima wawajibike kwani ni maazimio ya Bunge.
Ndugai alisema kanuni za Bunge zinataka wajumbe wa kamati husika wafanye uchaguzi, ndipo vikao vya kamati husika vitaendelea.

Post a Comment

Previous Post Next Post