Shein afuta michango, ada za mitihani

Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ametangaza kufuta michango kwa elimu ya msingi na gharama za mitihani kwa wanafunzi wa sekondari kuanzia Julai mwaka huu.
Dk Shein alitangaza uamuzi huo jana kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizofanyika kwenye uwanja wa Amaan mjini Unguja na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali mashuhuri akiwamo Rais Jakaya Kikwete.
Viongozi wengine waliohudhuria sherehe hizo ni Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, Spika wa Bunge, Anne Makinda, Jaji Mkuu, Othman Chande na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu.
Pia walikuwapo marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa na Kiongozi wa upinzani Bungeni, Freeman Mbowe pamoja na viongozi wengine wa vyama vya siasa Zanzibar.
Kufuta michango
Dk Shein alisema katika mwaka huu wa fedha, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imefuta gharama zote katika elimu ya msingi, sekondari pamoja na gharama za matibabu na upasuaji kwa wazee na wajawazito.
“Serikali yangu itaendelea kudumisha misingi na malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kuanzia mwaka huu wa fedha elimu ya msingi na sekondari itakuwa haina malipo, wazazi na wazee nao hawatachangia huduma zozote za matibabu na afya,” alisema Dk Shein.
Alisema tangazo la kutoa elimu bure lilitangazwa na Rais wa kwanza wa Zanzibar, hayati Mzee Abeid Karume Septemba 23, 1964 na hivyo hiyo ni kuendeleza misingi hiyo iliyoachwa na ASP ya elimu kwa wote hadi sekondari.
Uchaguzi Mkuu
Akizungumzia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba na Kura ya Maoni Aprili 30, mwaka huu, Dk Shein alisema lengo la SMZ na Serikali ya Jamhuri ni kuona shughuli hizo zikifanyika katika mazingira ya amani na utulivu na kuidhihirishia dunia kuwa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia.
“Serikali zote mbili zitaendelea kutimiza wajibu wake wa kulinda nchi na mipaka yake, zitahakikisha kuwa wakati wote zinakabiliana na vitendo vya uvunjifu wa amani. Vikosi vyetu vya ulinzi na usalama viko makini kusimamia jukumu hilo,” alisema Dk Shein.

Post a Comment

Previous Post Next Post