Sijui kama Wanakumbuka,leo ni januari 26,2015

Nawaamkua kwa heshima na taadhima. Baada ya kusubiri saa 48 za taarifa kutoka mjengo mweupe, kinachofuata ni mivutano ya hoja. Tunataraji kusikia hoja zikitoka Makao Makuu mjengoni kuanzia kesho.
Siyo nia yangu leo kuzungumzia siasa, ila ninataka kuzungumzia siasa zetu naweza kuziita za ubabaishaji, za zimamoto na kulaumiana.
Ninawiwa kusema hivyo kwa nini, mwaka huu tunajua kabisa kuna Michezo ya Afrika itakayofanyika kwenye mji wa Brazzaville, nchini Congo.
Ila natoa angalizo, imeelezwa katika kufuzu kwa michezo hiyo si kigezo cha kufuzu kwa Michezo ya Rio de Janeiro, Brazil mwakani. Kila hatua itakuwa na vigezo vyake kufuzu.
Uamuzi ulifikiwa na Shirikisho la Vyama vya Olimpiki Afrika (Anoca) na Umoja wa Afrika, AU katika mkutano wa 2013 kwamba Michezo ya Afrika 2015 ya Brazzaville isitumike kama kupata tiketi kwa Michezo ya Olimpiki ya Rio 2016.
Turudi kwenye ya kwetu. Michezo ya Afrika inatarajia itafanyika mjini Brazzaville kuanzia Septemba 4 hadi 19 mwaka huu. Mataifa 53 ya Afrika yanatarajia kupeleka wawakilishi wake, ikiwemo Sudani ya Kusini.
Hili la kwetu, bado najiuliza. hivi baada ya Michezo ya Afrika 2011 iliyofanyika Maputo, Msumbiji, vyama vya riadha, mikono, ngumi, wavu, soka, kikapu, netiboli kati yao, nani ameandaa wanamichezo wake kwa michezo ya Afrika ya mwaka huu?
Niliwahi kuandika kama haya, kwamba bado nayaona maandalizi ya zimamoto. Maandalizi ya wiki mbili kabla ya michezo ambayo tutamwita Rais na kumwambia wanamichezo wameiva tayari kwa michezo, halafu wanaenda kutia aibu.
Niliwahi kusema na ninarudia kusema, siioni hata medali ya Michezo ya Afrika 2015, lakini najua tutakwenda tu kushiriki.
Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Msajili wa Vyama vya Michezo na Klabu, Kurugenzi ya Maendeleo ya Michezo na Kamati ya Olimpiki Tanzania, (TOC), nashangaa na naendelea kuushangaa ukimya wao.
Ninafahamu huu ni uwanja wa Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo kuhakikisha mambo yanakwenda kwenye mstari.
Inatakiwa Serikali itekenye halafu isikilize, hawa watu wapo? Nini wanafanya? Kweli wanaandaa wanamichezo kwa michezo ya Afrika kama si Olimpiki na wakati mwingine Madola?
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post