TUJADILI LUGHA AU UBORA WA ELIMU?

LEO tunaimaliza rasmi Januari, kwa sababu watakaobahatika kuamka salama kesho, watakuwa katika mwezi mwingine ambao unathibitisha kwamba mwaka 2015 umeanza kukatika.
Binafsi, bado ninakumbuka siku ile ya Desemba 31, 2014 nilipolazimika kusubiri hadi saa sita na dakika moja usiku ili nipige yowe la kumshukuru Mungu kwa kuuaga vizuri.
Tofauti na miaka iliyotangulia, huu utakuwa wa kipekee kutokana na matukio muhimu yanayouhusu; kwanza ni upigaji wa kura ya maoni kuhusu katiba mpya inayopendekezwa na baadaye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Haya ni mambo ya kuzingatiwa sana kwa sababu hayana vyama vya siasa, ni ishu ya utaifa kwa vile yote yana uhusiano wa karibu sana na maisha yetu ya kila siku.
Leo nina mada mezani ambayo ni mjadala wa muda mrefu katika jamii yetu, ingawa kwa bahati mbaya sana, umekuwa hauwahusishi wahusika, kwa maana ya wanafunzi wenyewe ili nao watoe mawazo yao. Zipo hizi kelele zinazopigwa kuhusu lugha gani hasa inafaa kutumiwa katika masomo kwenye shule zetu, hasa kuanzia msingi hadi sekondari.
Watu wa kisasa wanapigia debe kutumika kwa lugha ya Kiingereza, wakiwa na hoja nzuri kabisa kuwa ni vyema tukaitumia hii kwa sababu inatambulika na kutumika kimataifa, wakati watu wa aina yangu, bado wanaamini katika kutumia Kiswahili, kwani licha ya kueleweka vizuri miongoni mwa Watanzania wote, pia ni mojawapo ya njia za kuipromoti ili nayo itambe duniani.
Ipo kasumba miongoni mwetu ya kuamini kuwa mtu anayezungumza Kiingereza ni msomi. Ndiyo maana hata leo, wazazi wanaowapeleka watoto wao katika shule za Academy, wakiwasikia wanazungumza maneno mawili matatu ya Kiingereza, wanaamini vijana wao wana akili, wanashangilia na kutembea kifua mbele. Kitu ambacho tunashindwa kuelewana baina ya makundi haya, kiasi cha mimi kuomba uhusika wa wanafunzi, ni uelewa wa tunachobishania. Wanaoshabikia umombo wana hoja za lugha ya kimataifa, wakati wamatumbi tunamaanisha kuelewa kinachofundishwa.
Sipingi Kiingereza, lakini je, vijana wetu wanaelewa masomo wanayofundishwa? Hofu yangu ni kuwa mwisho wa siku tutakuwa na vijana wengi wanaojua ung’eng’e lakini vichwa vyao vikiwa vitupu katika ufahamu wa mambo. Kwa nini kwa mfano, kijana wa Mikumi afundishwe kwa Kiingereza juu ya mbuga za wanyama zinazomzunguka wakati angeelewa vizuri zaidi kama ungetumia lugha ya taifa?
Vipo vitu vya kujifunza kwa lugha za watu, lakini upo umuhimu mkubwa wa kuenzi lugha yetu. Tunatakiwa kufundishwa masomo ili tuyaelewe, baadaye lugha hizi za kibiashara zifuate. Wachina hawajawahi kuipa kipaumbele lugha yoyote nje ya kikwao, lakini wanakamata nafasi za juu katika mambo mengi duniani, yakiwemo ya kiuchumi, kijeshi na maendeleo ya viwanda.
Leo hii, unalazimika kwanza kujifunza lugha za Kichina ili uweze kushughulika nao vizuri, vinginevyo itakula kwako. Lakini hili halijawazuia Wachina kujifunza Kiingereza wala lugha nyingine za kimataifa. Ninajua, kasumba na historia itatukataza kuepuka matumizi ya umombo katika shule zetu, lakini upo ulazima mkubwa sana wa kuhakikisha lugha hii inapata kipaumbele cha kufundishwa mashuleni, ikibidi zaidi kuliko ilivyo kwa Kiingereza.
Hii ni kwa sababu ukiondoa somo la Kiswahili kama somo darasani, katika shule hizi za Academy, hakuna somo lingine linalofundishwa kwa lugha hii, wakati upo ukweli kuwa Kiswahili kinachotumika mitaani na mashuleni, kina makosa mengi ya kisarufi na maana tofauti na ilivyo!

Post a Comment

Previous Post Next Post