Uraisi,jukumu linalogeuzwa kazi rahisi Tanzania

Kwa kuhesabu kwa vidole vyako vya mkononi tu, hautawapata marais wengi bora wa Marekani na kumwacha kando James Knox Polk.
Huyu ni Rais wa 11 wa Marekani aliyeahidi kuitawala kwa muhula mmoja tu wa miaka minne na kweli akafanya hivyo kati ya 1845 hadi 1849.
Wanazuoni wanamchukulia Polk kama mmoja kati ya marais bora kuwahi kuiongoza Marekani. Alikuwa mtaalamu wa kupanga sera zake na kuzitekeleza kwa vitendo. Alikuwa rais imara zaidi wa Marekani kabla ya vita mbili kuu za dunia.
Alikufa kwa kipindupindu miezi michache tu baada ya kuondoka madarakani.
Lakini kabla ya kifo chake, Polk aliwahi kutoa kauli maarufu ambayo inabeba ukweli ambao kwa sasa unadharauliwa kihisia katika nchi inayoitwa Tanzania.
Polk aliwahi kusema; “With me it is exceptionally true that the Presidency is no bed of roses.” Kuna sentensi nyingi zinazoweza kufafanua dhamira ya alichosema, lakini sentensi ya haraka zaidi unayoweza kuitumia ni kwamba ‘Urais sio kazi rahisi’.
Taifa lenye nguvu
Ndani ya taifa lenye nguvu za kiuchumi kama Marekani, urais unaonekana kuwa kazi ngumu. Lakini ndani ya Taifa maskini; linaloendesha maendeleo yake kwa kutegemea zaidi hisani ya wahisani, uraisi unaonekana kuwa kazi nyepesi sana.
Tunaendelea kusikia majina ya watu waliotamka au wanaotajwa kutaka kugombea urais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mengi kati ya majina haya ni mzaha mwingine mkubwa unaotunyemelea baada ya mizaha mingi ambayo tunahangaika nayo katika maisha ya kila siku.
Ndani ya ufunguo wa chama tawala, kuna ‘marais watarajiwa’ ambao wana kashfa kubwa za kukwapua mamilioni ya fedha za umma siku za nyuma.
Kuna walio madarakani ambao wanashutumiwa kutotimiza majukumu yao katika ubora au malengo tuliyojiwekea.
Kuna watu ambao hawana hata mizizi katika kuongoza wizara zao au majimbo yao ya uchaguzi, lakini wameingia katika msafara wa kenge. Tutasikia majina mengi kadri Januari itakavyoisogelea Februari na Februari itakavyokuwa inaiendea Machi.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post