Vinara wa Maandamano UDOM Watimuliwa - Waziri mkuu ( Mwakibinga ) Kafukuzwa Moja kwa moja


Wanafunzi watatu ambao wanatuhumiwa kuwa vinara wa maandamano ya wanafunzi wa programu maalumu ya walimu wa sayansi Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wameachishwa masomo.

Wakati mmoja wao akiwa amefukuzwa moja kwa moja, wawili wengine wana nafasi ya kujieleza kuhusika kwao na maandamano hayo, yaliyochafua hali ya hewa na kusababisha wanafunzi 84 kutiwa mbaroni.
 
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Idrisa Kikula akizungumza na Mpekuzi alisema kwamba watu hao wameondolewa jana asubuhi chini ya ulinzi wa polisi ili kurejesha utulivu katika chuo hicho.
 
Hata hivyo, alisema hadi jana wanafunzi wote wakiwemo hao wa program maalumu ya ualimu chuoni hapo walikuwa wanaendelea na masomo yao kama kawaida.
 
Aliwataja walioondolewa shuleni hapo kuwa ni Kyambwene Msatu (Rais), Philip J Mwakibinga (Waziri Mkuu) na Ismail Chande (Katibu Mkuu).
 
Alisema Mwakibinga amefukuzwa moja kwa moja, kutokana na kiapo chake alichokitia saini  baada ya vurugu za mwisho katika chuo hicho, kwamba hatajihusisha na uongozi na akirejea tena kutoa hamasa ya wanafunzi kugoma na kuandamana, afukuzwe moja kwa moja.
 
Alisema pamoja na hatua hizo zilizochukuliwa, wanaendelea na uchunguzi na wahusika wengine, kwani wamefanya mambo kinyume na taratibu za chuo na serikali.
 
Alisema Chuo kiliwaeleza wanafunzi bayana kwamba kama wana kitu, wafuate taratibu ili Chuo kiwasilishe malalamiko yao kwa mfadhili wao, ambao ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
 
Hata hivyo,  alisema hawakufuata na baadaye kuanza kuwa na mikutano haramu na kuamua kuandamana usiku huku wakiwashinikiza wenzao kwa kuwapiga kama hawatashiriki.
 
Juzi katika maandamano  hayo, polisi walisema kwamba wamekamata wanafunzi 84 ambao walikuwa wakiandamana kutoka chuoni hapo kuelekea katika Ofisi za viongozi wa Serikali zilizopo Dodoma mjini majira ya saa 11 alfajiri.
 
Profesa Kikula alisema wakati  maandamano hayo yanafanyika kwa bahati ilikuwa siku ya  baraza kamili la vyuo, ambalo limeridhia hatua zilizochukuliwa dhidi ya wanafunzi hao watatu, zilizolenga kuwapisha wenzao kuendelea na masomo.

Post a Comment

Previous Post Next Post