Viongozi wa dini watakiwa kujiweka kando na siasa.

Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muabhi
Vyama 10 vya siasa visivyokuwa na uwakilishi bungeni, vimewaonya  viongozi wa dini nchini katika kipindi cha mwaka huu wa uchaguzi mkuu kutojihusisha na masuala ya siasa kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Aidha, vyama hivyo vimeitaka serikali kupitia upya mikataba ya kampuni zinazozalisha umeme kwa kuwa baadhi zinauza nishati hiyo kwa gharama kubwa licha ya kwamba baadhi zinazalisha umeme kwa kutumia gesi na kusababisha wananchi kuingia gharama kubwa.

Tamko hilo lilitolewa na makatibu wakuu wa vyama vya AFP, CCK, SAU, UMD, Chausta, UPDP, NRA, Jahazi, Chauma na DP ikiwa ni salamu za kukaribisha mwaka mpya wa 2015.

Katibu Mkuu wa AFP, Rashid Rai, akisoma tamko hilo jana jijini Dar es Salaam kwa niaba ya wenzake, alisema katika miaka ya hivi karibuni ijitokeza tabia ya baadhi ya viongozi wa dini kujihusisha na masuala ya siasa hususani kipindi cha uchaguzi mkuu na kuwachanganya wananchi.

Rai alisema viongozi hao wamekuwa wakitoa matamko kwenye vyombo vya habari kupendekeza au kutoa sifa ya kiongozi anayefaa kuongoza nchi au asiyefaa kupewa nafasi ya uongozi wa umma katika Taifa.

Alisema viongozi wa dini lazima watambue kuwa sheria inazuia viongozi wa dini kujihusisha na masuala ya siasa kwani hali hiyo inawachanganya wananchi kushindwa kujua kama viongozi hao wamebadilisha majukumu yao.

“Unakuta kiongozi wa dini anasema Rais ajaye awe ni mwadilifu na mcha Mungu, au anasema  kiongozi huyu ni chaguo la Mungu, maana yake ni nini, kila dini au dhehebu lina vigezo vyake vya uadilifu na ucha  Mungu,” alisema.

Rai alisema kama viongozi wa dini wanaona watu waliopo kwenye siasa wanafaidi sana ni bora wakaachana na masuala ya kuhubiri dini badala yake waanzishe vyama vya siasa au wajiunge na vyama vya siasa ili waendelee kupata neema wanayohisi inapatikana huko.

Katibu Mkuu wa Sau, Ali Kaniki, alisema sakata la akaunti ya Tegeta Escrow limetoa fundisho kwa serikali kuona umuhimu wa kupitia upya mikata ya kapuni zote zinazozalisha umeme.

Alisema baadhi ya kampuni zinazozalisha umeme na kuliuzia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) zinatoza tozo kubwa, hali ambayo imekuwa ikisababisha gharama za umeme kuwa kubwa nchini.

“Tunazo kampuni zinazozalisha umeme hapa nchini ambazo ni Songas, IPTL Aggreko na Symbion, ukiangalia zote IPTL ndiyo inayouza umeme kwa bei ndogo ukilinganisha na nyingine, tunataka serikali ipitie mikataba ya kampuni hizo,” alisema.

Naye Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muabhi (pichani), alisema baadhi ya kampuni licha ya kutumia nishati ya gesi kuzalisha umeme, lakini zimekuwa zikiuza umeme kwa bei ya juu.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post