Wadau: Biashara ya sanaa bado wizi mtupu

Dar es Salaam. Licha ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuahidi kuwasaidia wasani katika kudhibiti wizi wa kazi zao, wadau wa sanaa nchini wamesema kuwa hawaridhishwi na adhabu zinazochukuliwa na vyombo vyenye mamlaka ya kulinda na kutetea haki za wasanii nchini.
Kutokana na kukithiri kwa wizi na uchakachuaji wa kazi za wasanii, wadau hao wameitaka Serikali kuingilia kati kwa kuwachukulia hatua zinazostahili kisheria wale wote watakaobainika kuhujumu wasanii.
Mbali na kutoridhishwa na hatua zinazochukuliwa pia wamewataka wasanii kufanya kazi zao kwa weledi na ubunifu kwa kuingia darasani na kuacha tabia ya kulipua kwa lengo la kufanya biashara.
“Sanaa ni kazi kama kazi nyingine, kazi ya msanii inahitajika kuheshimiwa na kulindwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zake na kwa wale wote watakaobainika kuwa wanaihujumu wadhibitiwe na kuwajibishwa,” anasema Edwin Semzaba.
Semzaba ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alieleza hayo wakati alipokuwa akitoa mafunzo kwa vijana toka vikundi vitatu vya sanaa ya maigizo vya Malezi Youth Theatre, Lumumba na Parapanda.
Anasema kwa hapa nchini bado mchango wa taaluma katika sanaa ya maonyesho siyo nzuri, hasa ikizingatiwa kuwa watu wengi wanaamini kuwa ni kipaji hata bila ya kuwa na elimu kitu ambacho siyo kweli.
“Kuna tofauti kubwa kati ya mtu mwenye kipaji na mtu aliyepata mafunzo, kwa kuwa aliyepata mafunzo ana wigo mpana wa kufanya shughuli zake tena kwa ubora kuliko yule mwenye kipaji lakini hana mafunzo,” alibainisha Semzaba.
Semzaba ambaye ni mwandishi wa vitabu, mwigizaji wa Sanaa za Maigizo na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi Vitabu nchini (Uwavita) anasema sanaa ya maigizo ni ngumu na yenye gharama, ikilinganishwa na sanaa za filamu licha ya kuwa inafanya vizuri.
Alisisitiza kuwa iwapo Serikali ingeweka sera madhubuti ambayo itasaidia kulinda na kudhibiti wizi na uchakachuaji wa kazi za wasanii nchini ingeweza kuwainua wao kiuchumi pamoja na pato la taifa kama ilivyo kwenye nchi za wenzetu.
Lakini kutokana na kuwapo kwa ukosefu wa sera hiyo madhubuti wasanii wamekuwa wakilia na kuingia hasara kutokana na kazi zao kuibwa na kuchakachuliwa kila kukicha.
Semzaba ambaye ni mtunzi wa kitabu cha Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe, anasema ili mtu awe msanii mzuri katika tasnia ya Sanaa ambayo inakuwa kwa kasi ni lazima apitie mafunzo ili aweze kufanya kazi zake kwa ufanisi na weledi.
Anasema moja kati ya vitu vinavyosababisha kazi nyingi za wasanii kushindwa kufanya vizuri katika soko la kimataifa, ni kutokana na kufanya kazi zao chini ya kiwango kwa kujikita zaidi kwenye biashara (masilahi zaidi) bila ya kuzingatia maudhui ili kazi iwe na ubora unaohitajika.

Post a Comment

Previous Post Next Post