Geita. Wakulima wa mananasi katika Kijiji cha Igate, mkoani
Geita wamesema kukosekana kwa soko la uhakika wa zao hilo, kunasababisha
hasara na kuwavunja nguvu.
Aidha, ukosefu wa ghala la kuhifadhi matunda na
mbogamboga katika eneo lao, nalo ni miongoni mwa sababu zinazowakatisha
tamaa kuendelea kulima zao hilo.
Malalamiko hayo yalitolewa jana wakati wa uzinduzi
wa ghala la kuhifadhi matunda na mbogamboga lililojengwa kwa ufadhili
wa Shirika la Maendeleo ya Wakulima Wadogo (ACORD).
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Emmanuel Simon
alisema asilimia 35 ya mananasi huharibika kila mwaka kutokana na
kukosekana sehemu ya kuyahifadhi.
Alisema wakulima wanakosa hamasa ya kulima mananasi kutokana na hofu ya kupata hasara.
“Wananchi wengi wa Igate tunategemea kilimo cha
mananasi. Ikumbukwe kuwa mananasi yanayolimwa hapa yanashika nafasi ya
kwanza kwa ubora katika soko la dunia,” alidaiSimon.
Alisema pamoja na ubora wa zao hilo, bado wakulima hawafaidiki vya kutosha kutokana na mananasi kuharibika
“Mananasi yanakaa juani muda mrefu, yananyeshewa na mvua na kukumbana na hali ya joto, hivyo kuharibika mapema,” alisema.
Akitoa mfano, alisema kwa jumla wakulima katika
eneo hilo wanazalisha tani 27,600, na mkulima mmoja anayezalisha tani
900, anapata hasara kwa sababu kati ya hizo, tani 200 huharibika.
Alisema mbali na tatizo la kukosa eneo maalumu la
kuhifadhi zao hilo, pia kukosekana kwa soko la uhakika kumechangia
kuwarudisha nyuma.
“Hatuna soko la uhakika la mananasi, hali hii imechangia kutuweka kwenye wakati mgumu zaidi,” alisema.
Akizindua ghala lenye thamani ya Sh53 milioni,
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Fatma Mwassa aliwashukuru wafadhili kwa uamuzi wa
kujenga ghala hilo la kuhifadhi matunda na mbogamboga. Mwassa alisema
kujengwa kwa ghala hilo, kutawashawishi wakulima wengi kuingia kwenye
kilimo cha zao hilo.

Post a Comment