Baadhi
ya wafuasi wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa wamerudia njiani
baada ya kupata taarifa za kutokuwapo kwa sherehe ya kupokea mwaka mpya
ambayo hufanyika kila mwaka nyumbani kwake Monduli ikijumuisha mamia ya
watu kutoka ndani na nje ya nchi.
Lowassa amekuwa akifanya sherehe hiyo kwa zaidi ya miaka mitano lakini mwaka huu hakufanya kutokana na kutumia adhabu ya CCM.
Msaidizi
wa Lowassa, Aboubakar Liongo alisema juzi kuwa mwaka huu, sherehe
hazikufanyika kutokana na Lowassa kuwa katika adhabu ya CCM inayomzuia
kukutana na idadi kubwa ya watu ili kuepuka kuonekana ni sehemu ya
kampeni.
Lowassa anatumikia adhabu ya miezi 12 ya kutoshiriki masuala yanayoashiria kampeni itakayomalizika mwezi ujao.
Wengine
katika kifungo hicho, ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri
wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Stephen
Wasira, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge
wa Sengerema, William Ngeleja. Alisema kama kuna watu waliofika
Monduli, walikuwa hawana taarifa za kutokuwapo sherehe hiyo ambayo
wameizoea kila mwaka.
Katika
sherehe kama hii mwaka jana, Lowassa alitangaza kuanza safari ya
matumaini ambayo alieleza itawezesha kupatikana huduma bora za afya na
elimu bure. Hata hivyo, alisema safari hiyo imejaa miba na mabonde na
kuwataka wanaomuunga mkono, kusimama kuhesabiwa. Tamko hilo, lilizua
mjadala nchi nzima na baadhi wakahusisha na safari ya urais.
Mwenyekiti
wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja katika hotuba yake, alipinga
tabia ya baadhi ya wanasiasa kutaka kuwachagulia marafiki.
Mmoja
ya wananchi waliokuwa safarini kwenda Monduli, John Kaaya mkazi wa
Arumeru, alisema walikuwa hawana taarifa za kutokuwapo kwa sherehe hiyo
ambayo alisema amekuwa akiihudhuria kwa miaka miwili.
Post a Comment