Wasanii walamba zaidi ya Sh150 milioni shoo ya Tigo

Huenda ukurasa mpya ukawa umefunguka kwa wanamuziki wa Tanzania baada ya kampuni ya mawasiliano ya simu za mokononi ya Tigo kumwaga zaidi ya Sh150 milioni kulipa wasanii 30 waliotumbuiza katika Tamasha la tiGOMusic Kiboko Yao Jumamosi iliyopita.
Habari ambazo gazeti hili imezipata, msanii aliyelipwa fedha kidogo kuliko wote, alitia kibindoni Sh5 milioni, lakini nyota wenye mvuto walilamba Sh70 milioni.
Kwa kiwango cha chini, iwapo kila mwanamuziki angepata Sh5 milioni tu, basi jumla ya Sh150 zilitumika kulipa wasanii kwa onyesho moja tu.
Hata hivyo siyo Kampuni ya Tigo, wala wasanii wenyewe waliokuwa tayari kuzungumza kuhusu malipo halisi waliyopata.
Pia, tofauti na maonyesho mengine ambayo wasanii hutumbuiza bila ya kusindikizwa na wacheza shoo au wasanii wenzao, Jumamosi ilishuhudia waburudishaji hao wajitahidi kuhakikisha wanaenea jukwaani.
“Jamaa wamejitahidi kutaka kuona tunatabasamu na ndio maana ukaona kila mtu anajitahidi kufanya kitu bora kuliko vyote alivyowahi kufanya katika huu muziki,” aliweka wazi Fid Q, ambaye jina lake halisi ni Fareed Kubanda.
Fid Q alipanda jukwaani na wasanii wenzake watatu na kuleta ladha tofauti na anavyofanya katika matamasha mengine yaliyopita.
Young Killer, Stamina na Tifah walikuwa ni wasanii walioshirikiana na Fid Q katika kufungua ukurasa wa Hip Hop katika tamasha hilo lililokuwa na lengo ya kuzindua mpango wa kupakua nyimbo za wasanii kupitia mtandao wa simu uitwao Deezer.
Msanii mwingine ambaye alipanda jukwaani tofauti na alivyozoeleka ni Ben Pol, mshindi wa tuzo ya Kili katika miondoko ya R&B, aliyepanda na madansa wazungu.
Hawa walikuwa wakicheza muziki wake wakati mwenyewe akiimba, hali iliyosababisha shangwe kutoka kwa mashabiki ambao walizoea kumuona Ben Pol akiimba peke yake jukwaani.
Mtaribu wa tamasha hilo, Alex Galinoma wa Kampuni ya East Africa TV LTD, alikiri kuwa kulikuwa na azma ya kuhakikisha wasanii wa nyumbani wanalipwa vizuri na walitekeleza hilo.
“Hayakuwa malipo ya kawaida waliyoyazoea... Hakuna msanii aliyelipwa hela aliyoizoea. Tulijitahidi kwenda juu, zaidi ya ile kawaida,” alisema Galinoma.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post