Dar es Salaam. Kesi ya ugaidi inayowakabili viongozi 23 wa
Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu sasa kusikilizwa na Hakimu Mkazi Janeth
Kaluyenda.
Awali kesi hiyo ambayo itatajwa Januari 13,2015
kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la ilikuwa
ikisikilizwa na Hakimu Mkazi, Hellen Liwa ambaye hata hivyo alijitoa.
Ni baada ya wakili wa washtakiwa hao wa ugaidi,
Abubakar Salim kumtaka ajitoe kuisikiliza kesi hiyo ili iweze kupangiwa
hakimu mwingine ambaye atatoa uamuzi juu ya hoja zao walizozitoa
mahakamani hapo Septemba 19,2014.
Washtakiwa wanaokabiliwa na kesi hiyo ya ugaidi ni
Sheikh Farid Hadi Ahmed ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa
Mbuyuni Zanzibar, Fundi Ujenzi mkazi wa Koani Zanzibar, Noorid
Swalehe na Jamal Nooridin Swalehe (38).
Nassoro Abdallah, Hassan Suleiman, Anthari Ahmed, Mohammed Yusuph, Abdallah Hassani, Hussein Ally na Juma Juma.
Saidi Ally, Hamisi Salum, Saidi Amour Salum,
Abubakar Mngodo, Salum Ali Salum, Salum Amour Salum, Alawi Amir, Rashid
Nyange, Amir Hamis Juma, Kassim Nassoro na Said Sharifu kwa pamoja
wanadaiwa kuwa walijihusisha na makosa hayo ya ugaidi kinyume na kifungu
cha 27(c) cha sheria ya kuzuia ugaidi ya 2002.
Wanadai kuwa kati ya mwezi Januari 2013 na Juni
2014 walipanga njama ya kutenda makosa hayo ya kula njama za
kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo vya kigaidi.
Katika kipindi hicho na maeneo tofauti nchini,
Sheikh Farid na Sheikh Mselem Mselem wanadaiwa kuwaingiza Sadick
Absaloum na Farah Omary nchini ili kushiriki kutenda makosa ya ugaidi.
Sheikh Farid anadaiwa kuwa kwa makusudi na
akijua alitoa msaada kwa watu hao wa kutenda vitendo vya kigaidi
kinyume cha sheria na kuwahifadhi.

Post a Comment