Dar es Salaam. Wakati Wazanzibari leo
wakiadhimisha miaka 51 ya Mapinduzi, wanasiasa na wasomi wametaka
wananchi hao kufanya mikakati muhimu ya maendeleo na kuacha fikra mgando
zinazoathiri maendeleo yao na nchi yao.
Wasomi na wanasiasa hao amesema Zanzibar imepiga
hatua kubwa za maendeleo kiuchumi, kijamii na kisiasa lakini zinaweza
kuendelezwa au kuharibiwa na Wazanzibari wenyewe iwapo wataendekeza
tofauti zao za kihistoria zinazohusiana na mapinduzi.
Zanzibar inaadhimisha sherehe hizo huku kukiwa na
matukio mawili makubwa ya kitaifa yanayoisubiri ikiwamo Kura ya Maoni ya
Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, ambayo kwa namna moja au
nyingine yanatajwa kuwa kipimo kikuu cha mwelekeo wa visiwa hivyo
kisiasa.
Maadhimisho hayo yatakayoongozwa na Rais wa
Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwenye Uwanja wa Amaan, yatahudhuriwa pia
na Rais Jakaya Kikwete na viongozi wengine waandamizi wa Serikali ya
Mapinduzi na ile ya Muungano.
Mhadhiri wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha
Zanzibar, Ali Uki alisema pamoja na kwamba Zanzibar imepiga hatua katika
ujenzi wa miundombinu, huduma za kijamii, sheria, kilimo na maendeleo
ya kisiasa kudumisha amani ndilo jambo la msingi.
“Suala la maendeleo hayo yamefikiwa kwa kiwango
gani? Kila mtu anatazama kwa jicho na mtazamo wake,” alisema Uki na
kuongeza kuwa kisiasa kuna mafanikio makubwa.
Alisema tangu kuanza mfumo wa vyama vingi mwaka
1992, Zanzibar imekuwa ikijitahidi kuhimili misukosuko mbalimbali ya
kisiasa ukiwamo upinzani mkali baina ya CCM na CUF uliosababisha kuundwa
kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Alisema mbali na mafanikio hayo, kuna haja ya
kufanya mkutano wa kitaifa wa kukubaliana kiwango cha sera za kufuatwa
kutoka katika kila chama kwani licha ya kuwa na SUK hivi sasa, sera za
CCM ndizo zinazofuatwa.
Iwapo itaonekana hili ni tatizo katika mwaka huu
wenye changamoto za Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu, Uki alisema kila
chama kinaweza kukaa katika kamati zake na wataalamu na kuamua kuhusu
kujumuisha sera zao ili kujenga mustakabali bora wa kisiasa Zanzibar.
“Watu waache fikra mgando kwamba hili ni suala
langu na lile ni la yule, wafanye maendeleo kwa ushirikiano kwa kuwa
mustakabali wa Zanzibar utatengenezwa na wao wenyewe,” alisema.
Mhadhiri katika Idara ya Sayansi ya Siasa ya Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alisema Mapinduzi ya Zanzibar
yana mafanikio makubwa na yameendelea kuwapo bila mapinduzi mengine,
jambo linaloonyesha yalikubalika vizuri.
Alisema mapinduzi yalifanikiwa kuendana na
misukosuko ya kisiasa ukiwamo mfumo wa vyama vingi vya kisiasa ulioleta
uga wa kisiasa usiotabirika wa nani atakuwa mshindi katika uchaguzi mkuu
wowote.
Post a Comment