Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu, tangu mwaka 2000 na 2010,
nilipata bahati ya kuhudhuria baadhi ya mikutano ya kampeni za wagombea
wa urais karibu wa vyama vyote.
Katika mikutano hiyo ya kampeni, miongoni mwa
mambo, waliyokuwa wanasema hasa wapinzani ni kuwa, Tanzania chini ya
mfumo wa sasa, hata kama Rais wa Marekani wakati huo, Bill Clinton akiwa
Rais wa Tanzania hawezi kuibadili kitu.
Kauli hii, wengi hatukuielewa lakini jambo moja
ambalo lilifafanuliwa ni kuwa Tanzania ina tatizo la mfumo wa uongozi na
hivyo yanahitajika mabadiliko makubwa. Mwanasiasa mmoja maarufu
alitueleza kuwa ili nchi hii iweze kuwa na maendeleo mazuri, inahitaji
mabadiliko ya kimfumo.
Akasema tuna matatizo lakini viongozi hawataki
kubadilika. Mfano mtu ameteuliwa kuwa kiongozi kila siku anakwenda
ofisini na kurudi nyumbani hana ajenda. Mwanasiasa huyu, akasema
kiongozi huyu wa serikali kila siku anategemea kufanya kazi kutokana na
matukio, akipigiwa siku kuna vurugu sehemu fulani anakwenda kusuluhisha,
kisha anarudi ofisini bila kufikiri ajenda ya kumaliza vurugu.
Kauli za wanasiasa hao naamini zina ukweli fulani
katika kupata mwarobaini wa matatizo ya Taifa letu ambalo mengi
tulipaswa leo yawe ni historia.Miaka zaidi ya 40 iliyopita, Baba wa
Taifa, hayati MwalimuJulius Nyerere alisema nchi ikitaka kuwa na
maendeleo inapaswa kuwa na ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Wapo
mawaziri ambao wameondolewa hadi sasa “wanalia” hawajui makosa yao,
lakini walibanwa wawajibike kutokana na kuziongoza wizara ambazo kuna
watendaji wa chini wanafanya makosa.
Katika wizara moja tu ya Nishati na Madini kuna
orodha ndefu ya mawaziri ambao wameondolewa kwa aibu. Katika Serikali ya
awamu ya nne pekee mawaziri wanne wamepitia wizara hii na kuingia
matatani.
Mawaziri hawa ni Nizar Karamagi, Dk Ibrahim
Msabaha, William Ngeleja na sasa Profesa Sospeter Muhongo ambaye kwa
sasa amewekwa kiporo kwa kashfa ya Escrow.
Hata hivyo, katika kashfa zote ambazo zimekuwa
zikiwakabili mawaziri hawa kumekuwapo na utata wa kuhusika kwao moja kwa
moja kijinai. Nadhani wizara hii moja inatosha kutufikirisha tuna
tatizo gani? Ukijiuliza swali hilo, unaweza kupata miongoni mwa majibu
ni mfumo wa uongozi wetu. Haiwezekani kufanyika ufisadi na kuchotwa
zaidi ya Sh300 bilioni katika mazingira tata, wakati Taifa lina vyombo
vingi vya usalama. Hapa ndipo unanipa jibu kuwa ni kweli hata kama
Clinton angepewa wizara hii angefukuzwa.
Wizara kama hii moja tu, waziri huyo, amezungukwa
na washauri wanaotambulika kisheria. Hawa ni kama vile katibu mkuu,
manaibu makatibu wakuu, wakurugenzi wa bodi, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali na wakurugenzi wa idara mbalimbali. Mfumo huu, ndio naamini
uliisukuma hata iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya Jaji
Joseph Warioba, kutoa mapendekezo juu ya kupunguzwa mamlaka ya Rais,
ikiwapo uteuzi wa nafasi mbali mbali . Rais kwa sasa anateua mawaziri
wakuu wa mkoa na wilaya, wenyeviti wa bodi, wakurugenzi wa mashirika ya
umma na wenyeviti wa bodi, majaji, wakuu wa vyombo vya dola na wengineo.
Mfumo wetu mbovu pia naamini ulisaidia mapendekezo
ya kubadili utaratibu wa kupatikana mawaziri, kwa kupendekeza wasiwe
wabunge ili ipatikane fursa huru ya mawaziri kufanya kazi za Serikali na
pia kufika kuhojiwa bungeni wasiwe na masilahi na ubunge.
Binafsi naamini, ili Taifa liweze kubadilika,
umefika wakati kutazama upya mfumo wetu wa uongozi ili kutoa fursa
watendaji wenye mawazo mapya waweze kufanya kazi.
Hivyo, kama tunataka maendeleo katika Taifa letu ni lazima tukubali kubadili mfumo
- Mwananchi
Post a Comment