Ajiandalia MAZIKO Kwa Miaka 14 sasa Mkoani Rukwa

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mkazi wa mjini Namanyere mkoa wa Rukwa, Gilbert Paul (37) aliyejiandalia maziko yake miaka 14 iliyopita, bado yu hai.

Kwa sasa  mtu huyo ameanza maandalizi ya kuchimba na kujenga kaburi la gharama, ikiwa ni pamoja na kununua jeneza.
 
Paul, baba ya mtoto mmoja na mchoraji maarufu mjini Namanyere aliyehitimu Kidato cha Nne 2001 katika Shule  ya Sekondari Nkasi, anasema anafanya hivyo kwa kuwa ana amani maisha ya duniani yana ukomo wake na ni ya kupita tu.
 
Aliyasema hayo juzi, akithibitisha kujichongea msalaba mkubwa  na kuutundika kwenye paa  la kibanda chake  anamofanyia kazi zake  katika Mtaa wa Sasala.
 
Msalaba huo  mweupe  mkubwa,  umeandikwa  tarehe aliyozaliwa ya Desemba 24, 1977, lakini katika tarehe ya kufa, ameweka  alama ya kiulizo. Msalaba huo unaonekana waziwazi, kiasi cha wageni wanaopita eneo hilo, kudhani ni nyumba ya ibada.
 
Paul  alisisitiza kuwa msalaba huo uliofikisha miaka 14 sasa, ndio  utakaosimikwa katika  kaburi  lake,  ambalo  anatarajia kulichimba na kulijengea, akikadiria litamgharimu Sh milioni moja, sawa na gharama ya jeneza alilotarajia kulinunua.
 
“Nilipotafuta mafundi wanitengenezee  msalaba huu,  wote waligoma  wakidai ni uchuro na  hawajawahi  kusikia wala  kuona mtu akijifanyia maandalizi  yake  ya  maziko akiwa bado anaishi .
 
 “Mama alilia sana walipomtaarifu,  akidai katika ukoo  wa baba yangu na  wa kwake  hakuna aliyewahi kufanya  hivyo …Baba alifariki  nikiwa  na miaka saba, mwanzoni  watu  walidhani nina tatizo la akili na wengine waliamini nimeathirika kwa Ukimwi hivyo nimekata tamaa ya kuishi, lakini sivyo…“ anasema.
 
Alieleza kuwa katika  maisha yake yote,  hakuwahi kuwa na rafiki wa kike mjini humo  kutokana na  kujitengenezea msalaba  huo, unaomfanya  wamuogope sana, hadi kuona kuna ulazima wa yeye kwenda kijiji cha mbali  na hapo .
 
“Nilichumbia na kuoa chapuchapu  nikihofia  mke wangu mtarajiwa akibaini nimejitengenezea msalaba hatanikubali,“ alieleza.
 
Mke wa Paul, Paskaria Salvatory (25) akizungumzia tukio hilo, anasema kama angefahamu, kamwe asingekubali kuolewa naye.
 
“Si kawaida mtu kujitayarishia maziko yake mwenyewe akiwa hai. Nilibaini  mwezi mmoja baada ya kuolewa,  kwa kweli  nilishituka  sana,  pia wanawake  wenzangu  walikuwa wakinibeza na kuniita kwa majina ya kuudhi,  lakini sasa nimezoea na nimezaa naye mtoto mmoja mwenye umri wa miaka miwili. Mume  wangu ana akili timamu, ni mwenye huruma  na  anayejali familia“, alibainisha.

Post a Comment

Previous Post Next Post