Zanzibar. Spika wa Baraza la Wawakilishi
Zanzibar (BLW), Pandu Ameir Kificho amesema Sheria ya Kura ya Maoni bado
haijaridhiwa na Baraza la Wawakilishi kama masharti ya Katiba ya
Zanzibar yanavyoeleza.
Kauli ya Kificho imekuja ikiwa ni siku moja baada
ya Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) na Taasisi ya Utafiti na Sera za
Jamii Zanzibar (ZIRPP), kusema sheria imekiukwa katika utekelezaji wa
mchakato wa Mabadiliko ya Katiba baada ya Baraza la Wawakilishi
kutoridhia Sheria ya Kura ya Maoni Namba 11 ya Mwaka 2013.
Pia walidai kwamba Rais Jakaya Kikwete alivunja
sheria kutokana na hatua alizochukua za kutangaza tarehe ya kufanyika
Kura ya Maoni akiwa China, wakati jukumu hilo ni la Tume za Uchaguzi za
Tanzania na Zanzibar kwa mujibu wa Kifungu cha 5(1)(B) cha Sheria ya
Kura Maoni.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Ikulu, Salva Rweyemamu alisema juzi kuwa Rais ana washauri wake wenye
taaluma zao akisema kuna Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Katiba
na Sheria ambao wanamshauri kwenye masuala ya kisheria.
“Ifikie mahali watu waheshimu taaluma za wengine
na wajue kwamba ni nani ambaye ametoa agizo, siyo kwa sababu wao ni
wanasheria, basi wakae tu kikao na kusema ya kwao kwamba Rais alivunja
sheria,” alisema Rweyemamu.
Kificho alisema tangu kutungwa kwa Sheria ya Kura
ya Maoni na kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwaka
2013, haijafikishwa katika Baraza na kwamba suala hilo linahitaji
kuzingatiwa kwa kuhakikisha Sheria ya Kura ya Maoni inawasilishwa kabla
ya Kura ya Maoni Aprili 30.
Alisema sheria yoyote itakayotungwa na Bunge kabla
ya kutumika lazima iridhiwe na Baraza la Wawakilishi kama haina
uhusiano na mambo ya Muungano.
Alisema Kifungu cha 132(1) cha Katiba ya Zanzibar
ya Mwaka 1984 kimeweka sharti kuwa: “Hakuna sheria yoyote
itakayopitishwa na Bunge la Muungano ambayo itatumika Zanzibar hadi
sheria hiyo iwe ni kwa ajili ya mambo ya Muungano tu na ipitishwe
kulingana na maelekezo yaliyo chini ya vifungu vya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano.”
Alisema ni sheria mbili tu zilizotungwa na Bunge
na kuletwa Zanzibar kuridhiwa kabla ya kuanza kutumika; Sheria ya Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala bora na Sheria ya Kuunda Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
Hata hivyo, Kificho alisema kwamba Sheria ya kura
ya Maoni imetajwa katika Sheria ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo
iliwasilishwa Barazani na kupata ridhaa ya Baraza la Wawakilishi kabla
ya kuanza kutumika ikiwamo kazi ya kukusanya maoni ya wananchi. Pamoja
na kutajwa katika Sheria ya Tume ya mabadiliko ya Katiba, Spika Kificho
alisema inahitajika kuangaliwa kama inatosha kwa kutajwa katika sheria
nyingine au la ili kufikia matakwa na masharti ya Katiba ya Zanzibar ya
Mwaka 1984.
Kificho alisema kwamba Tume ya Uchaguzi ya Taifa
(NEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ndizo zenye jukumu la
kusimamia Kura ya Maoni.
Awali, Rais wa ZLS, Awadhi Ali Said alisema
maandalizi na matokeo ya kura ya maoni yatakuwa batili kutokana na
Sheria ya Kura ya Maoni kuwa bado haijaridhiwa na Baraza la Wawakilishi
kinyume na Katiba ya Zanzibar.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment