Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola amesema
atawashawishi wananchi wasikichague Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika
Uchaguzi Mkuu utakaofanyika nchini Oktoba mwaka huu ikiwa serikali
haitatekeleza miradi ya kupekeleka maji katika Wilaya ya Bunda mkoani
Mara na hasa jimboni kwake.
Lugola aliyasema hayo jana, wakati akichangia mjadala kuhusu
taarifa ya utekelezaji ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na ile
ya Kilimo, Mifugo na Maji baada ya kuwasilishwa bungeni jana.
Alisema mradi wa ujenzi wa bomba la maji kutoka Tamau hadi Bunda
ambao pia unakusudia kuvipatia maji vijiji vya Bulamba Bizimbwe na
Mwisenye umekuwa kizungumkuti kwa muda mrefu sasa.
Alisema inasikitisha kwenye kitabu cha taarifa ya Waziri wa Maji,
Prof. Jumanne Magembe haujaweka mradi huo na badala yake ameweka miradi
mingi ya kwenye jimbo lake.
“Na hata kwenye kitabu hiki cha taarifa yake Mheshimiwa Waziri,
Hakuna mradi huu wa maji ya Bunda, mradi mkubwa, lakini ukienda kwenye
miradi yake ya Same, Mwanga ndiyo imejaa kwenye kitabu hiki, kwa nini
nisiamini unafanya kazi kwa kupendelea maeneo yako, ” alisema Lugola.
Alisema wakazi wa Bunda wanahitaji maji hayo kutoka Ziwa Victoria
lilipo umbali wa kilometa 20 lakini mpaka sasa ni zaidi ya miaka sita
tangu mradi huo uasisiwe hawajapata.
Alisema kwa sasa taifa linaelekea kwenye uchaguzi ambao anaamini
CCM kitaendelea kushinda kwa kishindo kwa kuwa Rais Jakaya Kikwete
amefanya mabadiliko ya mawaziri ambayo alitaka sasa yawe ni mabadiliko
yenye tija.
Hata hivyo alimtaka Maghembe kufanya mabadiliko haraka ya miradi ya
maji kwa kuwa wakazi wa Bunda akiwemo mwenyewe hawatakubali kuipigia
CCM kura ikiwa hawatapata maji mpaka kufikia kwenye uchaguzi huo.
“Mheshimiwa Maghembe unao muda wa kufanya mabadiliko wananchi wa
Bunda hatutakubali, hatutakubali kupiga kura kwa Chama Cha Mapinduzi,
iwe ni udiwani, wabunge, hata mimi nitasema msinipigie kura, haiwezekani
zaidi ya miaka sita wananchi wanatumia maji taka, mradi umekwama pesa
hakuna,” alisema.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Kamati ya
Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mjumbe wa Kamati hiyo, Said Nkumba
alisema halmashauri nyingi nchini zina madeni makubwa kutoka kwa
makandarasi hivyo akashauri serikali itoe fedha kwa wakati kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi hiyo.
Kamati hiyo pia ilipendekeza serikali kuanza utaratibu wa kutumia
mita za maji kwenye taasisi zake ili kuepukana na tatizo sugu la
kutolipia ankara.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment