Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru)
imembadilishia hati ya mashtaka Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma
aliyekuwa akikabiliwa na shtaka la kupokea rushwa ya Sh 323 milioni toka
kwa James Rugemalira fedha ambazo ni sehemu ya fedha za Akaunti ya
Tegeta Esrow.
Katika hati mpya iliyosomwa leo na Mwendesha
Mashtaka wa Takukuru Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya
Kisutu, Emillius Mchauru aioneshi tena kuwa fedha zilizopokelewa na
Mujunangoma toka kwa Rugemalira ni sehemu ya fedha za Akaunti ya Tegeta
Escrow.
Swai kupitia hati hiyo mpya alidai kuwa Februari
5, 2014 Mujunangoma akiwa mtumishi wa serikali kama Mkurugenzi wa Huduma
za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa
Mujunangoma alipokea rushwa ya Sh Sh323 milioni kupitia akaunti yake
namba 00120102602001 iliyopo kwenye benki ya Mkombozi .
Alidai kuwa mshtakiwa huyo alipokea kiasi hicho
cha fedha kutoka kwa James Burchard Rugemalira, ambaye ni mshauri huru
wa kitaalamu, mkurugenzi wa VIP na mkurugenzi wa zamani wa Kampuni ya
Kufua Umeme ya IPTL kama tuzo kwa kushughulikia mambo ya ufilisi wa muda
wa kampuni hiyo.
Aliendelea kudai kuwa baada ya kujipatia kiasi
hicho cha fedha alishindwa kueleza maslahi yake kwa Katibu Mkuu wa
Wizara yake ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kwenye tume ya
maadili ya Viongozi.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Mujunangoma
ambaye anatetewa na mawakili Deo Ringia na Jamuhuri Johnson alikana na
upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi umekamilika na wapo tayari kwa
ajili ya kumsomea mshtakiwa huyo maelezo ya awali (PH) yanayohusiana na
shtaka hilo linalomkabili.
Wakili Deo Ringia alitoa taarifa mahakamani hapo
kuwa kutokana na uchambuzi walioufanya wameona katika kesi hiyo kuna
masuala ya Kikatiba ambayo wanapenda mahakama iyaangalie na kuyatolea
maelekezo. Baada ya kutolewa kwa taarifa hiyo Hakimu Mchauru
ameiahirisha kesi hiyo hadi Februari 24,2015 kwa ajili ya kuisikiliza
taarifa hiyo.
Awali
Shtaka la awali, Mujunangoma alikuwa akidaiwa kuwa
Februari 5, 2014 katika Benki ya Mkombozi iliyopo wilayani Ilala, Dar
es Salaam, akiwa Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi alipokea rushwa ya kiasi hicho cha fedha
kutoka kwa James Burchard Rugemalira kama tuzo kwa kushughulikia mambo
ya ufilisi wa muda wa kampuni hiyo fedha ambazo ni sehemu ya fedha za
Akaunti ya Tegeta Escrow.
Mshtakiwa huyo anayedaiwa kufanya kosa hilo,
kinyume na kifungu cha 15 (1)cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa, Namba 11 ya mwaka 2007 yupo nje kwa dhamana na akaunti yake
inayodaiwa kupokea rushwa toka kwa Rugemalira imezuiwa.
Post a Comment