Moshi. Rais Jakaya Kikwete, amesema tatizo la upungufu wa
madaktari nchini ni kubwa lakini akasema Serikali imejipanga na kuweka
mikakati kabambe ya kulitatua.
Rais alitoa kauli hiyo leo wakati akizindua jengo
la chumba cha upasuaji la hospitali ya Rufaa ya Mawenzi na kuweka jiwe
la msingi jengo la wodi ya mama na mtoto.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, kwa sasa daktari mmoja
anahudumia wagonjwa 30,000 na muuguzi akihudumia wagonjwa 23,000, idadi
aliyosema ni kubwa.
Alisema kwa Ulaya, daktari mmoja huhudumia
wagonjwa 5,000 na kwamba ili nchi iweze kuondokana na tatizo hilo, ni
kuzalisha madaktari wengi watakaofanya kazi nchini.
Kuhusu mapambano dhidi ya maradhi mbalimbali, Rais
Kikwete alisema kwa sasa serikali inajenga uwezo wa ndani wa kupambana
na magonjwa ukiwamo ugonjwa wa malaria.
Hata hivyo Rais Kikwete alisema ipo changamoto ya
baadhi ya wananchi kutumia vyandarua wanavyopewa, kwa ajili ya kufugia
kuku na kuweka kwenye bustani za mbogamboga.
Rais Kikwete alitumia uzinduzi huo kumwaga takwimu
za Afya nchini, ambapo alisema pamoja na jitihada za Serikali, bado
asilimia 49 ya wajawazito wanajifungulia nyumbani.
Alisema takwimu zinaonyesha vifo vya wajawazito
vimepungua kutoka 126 hadi 119 kutoka kwa kila akina mama 100,000 na
kuagiza kila zahanati kuwa na wodi ya kujifungulia akina mama
wajawazito.
Akizungumzia hali ya lishe nchini, Rais Kikwete
alisema hali sio nzuri na kubainisha kuwa asilimia 42 ya watoto nchini
wana shida ya udumavu huku mkoa wa Kilimanjaro ukiwa na udumavu wa
asilimia 28.
Alisema asilimia tano ya watoto wana ukondefu,
asilimia 16 wana uzito mdogo huku upungufu wa madini joto ukiwa ni
asilimia 35 na kwamba tatizo hilo ni kubwa nchini.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, upungufu wa madini joto mwilini husababisha magonjwa mbalimbali ukiwamo ugonjwa wa Goita.
Baada ya hafla hiyo, Rais Kikwete alikwenda
kufungua jengo la kitega uchumi la Shirika la Hifadhi za Jamii (NSSF)
ambalo ndilo jengo kubwa la kibiashara mkoani Kilimanjaro.
Post a Comment