Ni simanzi na majonzi katika kijiji cha Ndami, 
wilayani Kwimba ikiwa ni siku 40 sasa, tangu mtoto Pendo Emmanuel (4), 
atekwe na watu ambao hawajajulikana hadi sasa.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Mwandu Madirisha, anasema wananchi wake
 hawapo vizuri kiakili tangu aibwe mtoto Pendo na kwamba “hawaamini kama
 mtoto yule hajaonekana mpaka leo.”
Anasema kijiji hicho kina barabara kuu tatu zinazoingia na kutoka 
katika vitongoji vya Misasi, Nyahonge na Chibwiji, hali inayochangia 
kuwapo na ulinzi wa jadi (sungusungu).
“Hata hivyo, hawa sungusungu wanalinda katika njia zile kuu tu…siku ya tukio la kuibiwa mtoto 
Pendo, hakuna aliyefahamu wala kuhisi chochote kwani tumezoea kuishi kwa amani kwa miaka mingi,” anasema.
Anasema kutokuwapo kwa matukio ya ‘ajabu’ katika kijiji hicho, 
ndiko kulikochangia watu wasio wema kutumia nafasi hiyo kumuiba Pendo na
 kutoweka naye kusikojulikana mpaka sasa. Madirisha anasema wakati watu 
hao wanatekeleza unyama wao kwa Pendo, kijiji kilikuwa hakina uongozi 
licha ya kuchaguliwa na wananchi, kutokana na kuchelewa kuapishwa mara 
baada ya kufanyika uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa na 
vitongoji.
Mwenyekiti huyo anasema inawezekana watu hao walitumia hali hiyo 
kufanya ‘uhalifu’ wa kuvamia nyumba yao iliyopo mbali kidogo na barabara
 zinazolindwa na sungusungu.
“Naamini ni tukio la imani za kishirikina linalowahusu zaidi 
wafanyabiashara wa migodini pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali 
ambao wanahitaji madaraka,” anasema.
MAMA PENDO
Mama mzazi wa Pendo, Sophia Juma, ambaye kwa sasa amehamishwa 
katika makazi yake na kupelekwa wilayani Misungwi, hakuwa na mengi ya 
kusema kutokana na kumfikiria mtoto wake.
“Namkumbuka sana mwanangu, sielewi huko alipo kipi kimemtokea, 
lakini namwamini Mungu waliotenda jambo hilo, uso wa Mungu utawaumbua,” 
anasema Sophia.
Anasema siku ya tukio akiwa na watoto wake wawili akiwamo Pendo, 
walilala chumbani na muda wa saa 4:00 usiku, walishitukia watu wameingia
 ndani na kumchukua mtoto kinguvu na kutoweka naye.
Hata hivyo, mama huyo hakuweza kuzungumza sana kutokana na simanzi alizonazo kuhusu mwanaye. 
MAJIRANI
Shigilu Kuya (70), ambaye nyumba yake ipo umbali wa mita 100 toka 
alipoibwa mtoto Pendo anasema alikuwa msibani wakati watekaji wanatimiza
 azma hiyo.
“Nilipokuwa msibani na mwanangu, usiku wa manane nilipigiwa simu na
 kuambiwa mtoto wa jirani Pendo amechukuliwa na watu wasiojulikana … 
nilishtuka na kuishiwa nguvu kabisa,” anasema mzee Kuya.
“Nilikuwa namfahamu sana Pendo maana amekuwa akicheza hapa kwangu 
na wajukuu zangu, kutoonekana kwake kumetufanya tukose raha lakini 
tukiamini Mungu ipo siku watamuona tu,” anasema.
Mzee Kuya anasema licha tukio hilo kushughulikiwa na kikosi kazi 
cha polisi, naye amefanikiwa kuisaidia polisi kwa kuwekwa mahabusu 
kutokana na tukio hilo.
Hata hivyo, anasema hafahamu kwa nini mtoto huyo ameibwa kwani 
hajawahi kusikia kijijini hapo kutokea kwa matukio kama hayo kwa miaka 
yake yote aliyoishi.
Kwa upande wake, Ngollo Maduka (50), jirani wa alipokuwa akiishi 
mtoto Pendo na wazazi wake, anasema anashikwa na hofu kubwa akimkumbuka 
mtoto huyo kutokana na jinsi walivyokuwa wakiishi naye na kucheza na 
wajukuu zake.
“Hatuamini kama tumempoteza Pendo, lakini naamini vyombo husika 
vitafanya kazi zake kiufasaha kuhakikisha wanafahamika na kufikishwa 
katika sheria wahusika wote wa tukio hilo bila upendeleo,” anasema 
Ngollo.
VIONGOZI WA DINI
Mwinjilisti Hagai Mkumbo wa kanisa la AICT Ndami, kiongozi wa kanisa alilokuwa akiabudu mtoto Pendo na wazazi wake anasema:
“Pendo amekuwa mshirika wetu tangu wazazi wake wahamie hapa, tena 
walikuwa katika mafundisho ya ubatizo…tumehuzunika na kusikitishwa sana 
baada ya kusikia tukio hilo.”
Anasema baada ya kupata taarifa ya watu kumuiba Pendo, kanisa 
lilifunga na kuomba kwa ajili yake ili Mungu asaidie kupatikana kwake, 
na wanaamini atapatikana.
Anasema wakati wa tukio hilo, baadhi ya waumini walienda nyumbani 
kwao kutoa msaada ingawa ilikuwa ngumu kuonana na mama yake kutokana na 
kuwapo na polisi wengi waliokuwa wakilinda eneo la nyumba yao.
Hata hivyo, anasema walipopata taarifa ya kuhamishwa mama Pendo nyumbani kwake, walifarijika na kumshukuru Mungu.
Mkumbo anasema tangu limetokea tukio hilo, limekuwa likiwaumiza na 
kuwakosesha amani, ingawa wanaamini Mungu ataingilia kati jambo hilo na 
kuweza kupatikana kwake.
David Mashimba ambaye ni mzee wa kanisa hilo, anasema walikuwa 
wakihitaji kupata mawazo ya Pendo na mama yake, lakini wamekosa hilo na 
kubaki kutafakari zaidi.
“Walikuwa wameanza mafundisho kwa ajili ya kubatizwa, lakini 
shetani amechukua nafasi yake kwa kuwaondoa katika nyumba ya Bwana,” 
anasema Mashimba.
MKUU WA MKOA
Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, baada ya tukio hilo 
alitembelea kijiji cha Ndama kilichopo tarafa ya Mwamashimba wilaya ya 
Kwimba na kuzungumza na wananchi wake.
Mulongo alitaka kuwafahamu hatua iliyofikiwa na viongozi na wananchi katika kuwabaini waliotenda unyama huo kwa mtoto Pendo.
Anasema tukio hilo linasikitisha kwani halijawahi kutokea tangu 
2007 wilayani humo wakati lilipomkumba mwananchi mmoja wa wilaya hiyo 
akisafiri kwenda mkoani Shinyanga kwa shughuli binafsi.
“Kiburi cha watekaji kimo humu humu haiwezekani mtu kutoka mbali 
aje atekeleze tukio kijijini bila yakuwa na wenyeji, lazima kuna mtu ama
 watu walioshirikiana na wahalifu hao. Mbona mifugo inapoibiwa 
hupatikana, iweje mtu asipatikane,” anahoji Mulongo.
Hata hivyo, Mulongo pamoja na kutoa siku tano kwa waliofanya tukio 
hilo kupatikana, laini siku hizo zimeisha huku jeshi la polisi 
likiendelea kuwachunguza waliokamatwa kwa tuhuma hizo akiwamo baba mzazi
 wa Pendo, Emmanuel Shilinde.
MWENYEKITI WA ALBINO MWANZA
Mwenyekiti wa chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi mkoani Mwanza, 
Alfred Kapole, amesema chama kinasikitisha kuona wanadamu wakiwaua 
wenzao kama wanyama na bila woga wowote.
“Inasikitisha kuona miongoni mwa kesi 72 zilizopo mahakamani, ni 
tatu tu ndizo zilizotolewa hukumu, lakini zingekuwa kesi ya wanasiasa 
kama wabunge wanashindana masuala ya uchaguzi wangetoa hukumu muda 
mrefu. Lakini si kwa walemavu wa ngozi,” anasema Kapole.
Anasema hata kama wanadamu wanashindwa kutoa hukumu, Mungu 
atawahukumu na kutoa maandikio katika kitabu cha Biblia Takatifu, Mika 
3.3-7, kinachoelezea hukumu watakayopata watu walao nyama za watu bila 
woga. 
Mwenyekiti Kapole amewaomba wasamaria wema wanaofahamu alipo Pendo 
wamrejeshe ama hata kama wamemdhuru basi mwili wake upatikane kwa ajili 
ya matanga na waliotenda jambo hilo wahukumiwe.
UNDER THE SAME SUN
Mkurugenzi mtendaji wa shirika la kuwalinda watu wenye ulemavu wa 
ngozi (albino), Under the Same Sun (UTSS), lenye makazi yake Canada, 
Peter Ash, ameshangazwa na vyombo vya dola kushindwa kuwakamata wanunuzi
 wa viungo vya albino licha ya kutajwa na waganga na wauaji.
Ash anasema viungo vya albino vinanunuliwa kwa bei kubwa ambayo 
mwananchi wa kawaida hawezi, lakini vyombo vya dola vinapowakamata 
wauaji na kuwahoji wanaelekezwa waliowatuma, bado vyombo vya dola 
vinashindwa kuwakamata.
“Inashangaza kuona licha ya kukamatwa kwa waganga ama wapiga ramli 
na wauaji wa albino, wakihojiwa na kuwataja wanaowauzia, wanashindwa 
kuwachukulia hatua…hali hii ni mbaya kwani bila jamii kusimama yenyewe 
‘mchezo’ huo utanedelea,” anasema Ash.
POLISI MWANZA
Awali akizungumza na NIPASHE, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, 
Valentino Mlowola, amesema kikosi kazi cha polisi kinaendelea na kazi ya
 upelelezi ili kuhakikisha waliotenda unyama huo wanapatikana.
“Tuliwakamata watu 15 akiwamo baba wa mtoto Pendo, Emmanuel 
Shilinde, lakini katika mchujo uliopitishwa ni watu wanane 
wanaoshikiliwa na jeshi hilo mpaka sasa,” anasema Mlowola.
Anasema pia jeshi hilo limefanikiwa kuinasa pikipiki (bodaboda) iliyotumika kufanya unyama huo.
“Mlowola anasema licha ya kuendelea kuwahoji watu hao, lakini huo 
siyo mwisho kosa la jinai kutokana na kutokuwa na mwisho hata baada ya 
miaka 20 tukio hili litaendelea kuchunguzwa.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kufanya ushirikiano na polisi 
kwa kile wanachofahamu kuhusiana na kuibiwa Pendo huku akisisitiza jeshi
 lake likitangaza dau la Sh. milioni 3 kwa atakayefanikisha kupatikana 
kwake. 
Pendo ni miongoni mwa albino 74 waliopo wilayani Kwimba, huku akiwa namba tisa katika suala la kupatiwa ulinzi.
TAKWIMU
Takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa ni asilimia mbili  tu ya watu
 ambao huzaliwa na ulemavu wa ngozi ndiyo wanaosherehekea miaka 40 ya 
kuzaliwa kwao, huku takwimu hizo zikionyesha nchi za Afrika ni mtu mmoja
 kati ya 2,000 huzaliwa wakiwa albino wakati Marekani mtu mmoja kati ya 
17,000 huzaliwa na ulemavu wa ngozi.
Mauaji ya albino nchini yanaonekana kukithiri zaidi katika mikoa ya
 Kanda ya Ziwa kutokana na imani za kishirikina, yakifuatiwa na mauaji 
ya vikongwe tangu yaliposhamiri mwaka 2006/07.
     CHANZO:
     NIPASHE
    

Post a Comment