Jeshi
la Kujenga Taifa lilianzishwa Julai 10, 1963 na serikali kwa lengo la
kuwaweka pamoja vijana wa nchi hii na kuwapa malezi kuhusu uzalendo na
umoja ili kuondoa dalili za matabaka zilizoanza kujitokeza katika jamii
baada ya uhuru.
Baadhi ya sababu za kuanzishwa kwa JKT ni:
Kubadili fikra za vijana wa nchi hii kutoka ile hali ya ukoloni kutegemea nchi nyingine kuleta maendeleo.
Kukusanya nguvu za vijana wote wa nchi hii na kuzielekeza kwa umoja wao kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya taifa.
Kuwafunza vijana kujenga mshikamano na umoja wa kitaifa, ili kulinda uhuru wa Taifa lao.
Jeshi
la Kujenga Taifa linaunganisha vijana bila kujali itikadi zao, dini,
elimu, jinsia na mali ili kuwalea kuwa wazalendo kwa taifa lao na
kupenda kuitumikia nchi yao.
Pamoja na dhana ya
kufunzwa uzalendo, pia stadi mbalimbali za kazi hufundishwa kwa vijana
hao ili waweze kujiajiri, pindi wamalizapo mkataba yao ya kujitolea kwa
miaka miwili.
Serikali ilirejesha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa vijana wa kujitolea mwaka 2001, baada ya kusitishwa mwaka 1994.
Masharti ya Kujiunga na JKT kwa vijana wa Kujitolea
Kijana kabla ya kujiunga na JKT hutakiwa kuyajua masharti na kuzifahamu taratibu za kujiunga na kuelewa kuwa JKT halitoi ajira.
Moja
ya kipengele cha masharti ya kujiunga na JKT kinasema kuwa ‘Kwa kipindi
chote nitakachokua ndani ya Jeshi la Kujenga Taifa nitakuwa nafanya
mafunzo ya kijeshi na ya stadi za kazi na maisha, na baada ya mkataba
nitarejea nyumbani. Hivyo sitalidai Jeshi la Kujenga Taifa ajira, wala
kulitaka linitafutie ajira/kazi’.
Kipengele
hiki kinaainisha masharti ya makubaliano kati ya Jeshi la Kujenga Taifa
na kijana kabla ya kujiunga na kupatiwa mafunzo ya awali ya kijeshi.
Aidha,
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete pamoja na viongozi wengine mara kadhaa wamekuwa wakisisitiza
kuwa, JKT halitoi ajira.
Lakini hivi karibuni
wakati nchi inaelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge mwaka huu,
umezuka mtindo wa makundi ya vijana waliopitia JKT katika Operesheni
mbalimbali kuomba kuandamana kwenda Ikulu kudai ajira.
Madai
yanayopingana na dhana ya JKT na kauli ya Mhe. Rais kuwa Jeshi la
Kujenga Taifa haliajiri, bali vijana hujiunga kwa hiari kwa kujitolea na
baada ya mkataba wa miaka miwili wanatakiwa kurejea walikotoka.
Aidha, Mhe. Rais Kikwete, amewahi kutoa agizo kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, taasisi za Serikali na kuziomba zile zisizo
za kiserikali kutoa ajira kwa vijana waliopata mafunzo ya JKT kulingana na sifa za kijana na nafasi zilizopo.
Takwimu
zinaonesha kuwa tangu kurejeshwa kwa mafunzo ya JKT mwaka 2001 hadi
mwaka jana, jumla ya vijana 104,594 wamejiunga na JKT wakiwemo wavulana
76,832 na wasichana 27,762.
Katika kipindi
hicho, jumla ya operesheni 13 katika mafunzo ya JKT zimefanyika,
Operesheni hizo ni pamoja na Operesheni Mkapa mwaka 2001, Miaka 40 ya
JKT mwaka 2002, Utandawazi mwaka 2004 na Operesheni Jiajiri mwaka 2005.
Zingine
ni pamoja na Kasi Mpya mwaka 2006, Maisha Bora mwaka 2007, Uadilifu
mwaka 2008, Kilimo Kwanza mwaka 2009 na Operesheni Uzalendo mwaka
(2010), Miaka 50 ya Uhuru (2011), Sensa mwaka 2012, Miaka 50 ya JKT
(2013) na Miaka 50 ya Muungano (2014).
Vijana
wa Kujitolea walioajiriwaTangu mwaka 2003 hadi 2014 jumla ya vijana
24,708 wameajiriwa katika vyombo vya ulinzi na usalama ambapo vijana
21,977 wakiwemo wavulana 17,307 na wasichana 4,670 wameajiriwa na Jeshi
la wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Jeshi la Polisi
vijana 3,965 wavulana wakiwa 2,943 na wasichana 1,022, Magereza vijana
2,139 wavulana 2,044 na wasichana ni 95, Zimamoto vijana 100 wavulana
wakiwa ni 78 na wasichana ni 22 na taasisi zingine vijana 592 Vijana
1,622 wameajiriwa katika taasisi mbalimbali kama TANAPA, GEITA GOLD
MINE, BANDARI na AFRICAN GOLD MINE.
Ni vema
vijana hao wakatambua kuwa tatizo la ajira sio kwao peke yao, ni tatizo
la ulimwengu mzima Tanzania ikiwemo, wanashauriwa kutumia stadi za kazi
kujiajiri wenyewe.
Aidha, vijana hao watambue
kuwa walikula kiapo cha UTII, wakati wa kuhitimu mafunzo ya JKT, hivyo
suala la kuandamana ni kinyume cha kiapo chao. Vijana hao walitumikia
Jeshi la Kujenga Taifa Operesheni za nyuma na kumaliza mkataba wa miaka
miwili. Shinikizo lao la kulazimisha ajira kwa kuandamana ni kinyume cha
sheria za nchi.
Kwa maelezo ya hapo juu utaona
kuwa Jeshi la Kujenga Taifa, halina dhamana ya kuajiri bali kufunza
vijana wa taifa hili umoja, stadi za kazi na uzalendo baada ya hapo
wenye sifa za kuajiriwa hupata ajira katika taasisi mbalimbali za
serikari na binafsi.
Taarifa hii Imetolewa na
Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa.

Post a Comment