MAMLAKA
ya Mapato Tanzania (TRA) imewakumbusha wamiliki wa pikipiki maarufu
kama bodaboda kuzifanyia usajili kwani watakaoshindwa kufanya hivyo
ndani ya muda uliopangwa watachukuliwa hatua za kisheria.
“Tunawaomba na kutoa mwito kwa wamiliki wa pikipiki kutii sheria na kusajili namba mpya kabla Machi 31, 2015,”
alisema Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Mlipa Kodi wa TRA Richard
Kayombo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
jana.
TRA
ilitangaza kipindi cha miezi sita cha usajili wa namba mpya za pikipiki
kuanzia Oktoba 1, mwaka jana hadi Machi 31, mwaka huu kama sehemu ya
mpango mkakati wa TRA wa kuweka utaratibu mzuri wa kusimamia utoaji wa
namba za magari na pikipiki kwa kuzitenganisha.
Utaratibu wa namba mpya pia unalenga kuzuia wimbi la uhalifu, unaochangiwa na bodaboda. “Mwisho wa muda wa usajili wa namba mpya ni Machi 31, mwaka huu.
TRA
inatoa mwito kwa wamiliki wa bodaboda kusajili upya vyombo vyao kwa
hiari na kupata namba mpya, ambazo zinaanza na MC 101 AAA. Pikipiki za
biashara zinakuwa na pleti namba “nyeupe” wakati zile za kawaida
zinakuwa na namba za “njano.”"
Akielezea
kuhusu masuala mbalimbali yaliyoibuliwa wakati wa mchakato huo wa
usajili wa namba mpya za pikipiki, Kayombo alisema gharama ya
kubadilisha namba kutoka ya zamani kwenda mpya ni kiasi cha Sh 10,000
tu.
“Kwa
wale ambao hawajalipia leseni za barabarani watatakiwa kulipia kwanza
gharama hizo kabla ya kupata namba mpya. Na wale ambao hawajabadilisha
majina ya umiliki wa pikipiki watatakiwa kufanya hivyo kabla ya kupata
namba mpya.”
Kwa
mujibu wa Kayombo, TRA imesambaza maofisa wake nchi nzima kuwahamasisha
waendesha na wamiliki wa bodaboda kusajili pikipiki zao na kupata namba
mpya. “Elimu hii imeenda hadi chini kwenye vituo vya bodaboda.
Tumefanya
hivi katika mikoa yote ya Kodi katika jiji la Dar es Salaam (Ilala,
Temeke na Kinondoni), Pwani, Morogoro, Ruvuma, Njombe, Iringa na Mbeya.
Zoezi kama hili linaendelea Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa na Kanda ya
Kaskazini,” alisema.
Mfumo
mpya wa usajili wa pikipiki umekuja kama njia ya kuweka utaratibu mzuri
wa namba za magari na pikipiki kwa kuzitenganisha, alisema Kayombo, na
kuongeza kuwa mfumo huu pia utasaidia kupunguza matukio ya uhalifu
nchini, yakihusisha unyang’anyaji wa kutumia silaha na wizi
unaowahusisha waendesha pikipiki au bodaboda.
Pamoja
na kuongeza pato la serikali, Kayombo aliuelezea mfumo huo mpya kama
“mkakati madhubuti,” utakaolinda maslahi ya wamiliki wa pikipiki na
kusaidia Tanzania na watu wake kuondokana na vitendo vya kihalifu
vinavyohusisha pikipiki
Post a Comment