Wananchi walipendekeza madaraka makubwa ya Rais
hasa ya uteuzi yapunguzwe na ziundwe taasisi za kikatiba za kumshauri
rais kabla hajafanya teuzi. Wananchi walipendekeza pia baada ya rais
kumteua kiongozi basi itabidi mteuliwa huyo Bunge limthibitishe.
Katiba Inayopendekezwa imeyafuta haya yote na imemwongezea Rais madaraka.
2. Kutenganisha mamlaka ya mihimili ya dola
Wananchi walipendekeza uhuru zaidi kwa Bunge na
mamlaka zaidi kwa Bunge kuisimamia, kuiwajibisha na kuishauri Serikali.
Pendekezo hili linaenda sambamba na kutenganisha Serikali na Bunge, hali
ambayo iko sasa. Rasimu ya Warioba ililipa Bunge mamlaka zaidi
kuisimamia Serikali na hata pale ambapo Bunge lingekataa bajeti au
muswada mbaya wa Serikali mara kadhaa, rais asingeliweza kulivunja
Bunge. Wananchi walisema sana mawaziri wasitokane na wabunge, ili
wabunge wafanye kazi ya uwakilishi pekee na mawaziri watumie weledi wao
kumsaidia rais kazi za Serikali.
Katiba Inayopendekezwa imefuta masharti haya.
3. Kumwajibisha mbunge
Rasimu ya Warioba iliwapa wapiga kura uwezo wa
kuwawajibisha wabunge kwa kupiga kura ya kutokuwa na imani nao wakati
wowote kama wakienda kinyume na masilahi ya wananchi katika jimbo
husika. Wananchi walijiuliza kama mbunge ni mtumishi wao, iweje hayuko
katika kituo cha kazi kwa miezi kadhaa na wasiweze kumwajibisha mpaka
miaka mitano? Katiba Inayopendekezwa imefuta masharti haya.
4. Vyanzo vya mapato vya kuaminika
Kuwapo kwa vyanzo vya mapato vya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano vitakavyogharimia mambo ya Muungano ambayo
yamepunguzwa kutoka 22 hadi 7 lilikuwa pendekezo ambalo hata taasisi za
Serikali zilipendekeza. Katiba Inayopendekezwa imerudisha mapato ya
Muungano kama Katiba ya Mwaka 1977 na kwa kufanya hivyo tumerudi kwenye
mgogoro wa msingi, kuchukua kodi tatu, ushuru wa forodha, ushuru wa
bidhaa na mapato kutoka Zanzibar ni kuiua Zanzibar na kuifanya ishindwe
kumudu matumizi yake ya ndani kwa mambo yasiyo ya Muungano na vivyo
hivyo kwa Tanganyika.
5.Muundo wa shirikisho lenye mamlaka kamili
Kwa miaka nenda rudi tumekuwa na kitendawili cha
ni muundo gani wa Muungano Jamhuri yetu inao. Kitendawili hiki
kimeelezwa na wengi akiwamo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Rasimu ya
Warioba iliweka kwa mara ya kwanza Muundo Jamhuri ya Muungano kuwa ni wa
Shirikisho lenye Mamlaka Kamili, nchi moja na yenye Serikali tatu.
Kilichoongezwa ni na Rasimu ya Warioba ilikuwa Bunge na Serikali ya
Tanganyika na siyo nchi ya Tanganyika kama ambavyo wengi wameaminishwa
hivyo. Katiba Inayopendekezwa imerejesha na kuudhoofisha zaidi muundo wa
Serikali mbili, kwa kuifanya Tanganyika au Tanzania Bara kuwa ndiyo
Jamhuri ya Muungano na Zanzibar kuwa na mamlaka zaidi kwa mambo yasiyo
ya Muungano ikiwamo kujiunga na jumuiya za kimataifa.
- Mwananchi
- Mwananchi

Post a Comment