Ikiwa ni siku moja tangu Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
kutangaza kung’atuka katika nafasi yake ya ubunge, Bunge limeeleza kuwa
mbunge huyo atapata mafao yake yote kama wabunge wengine.
Zitto ambaye alitangaza juzi bungeni kuwa
anaondoka baada ya kuvuliwa unanachama wa Chadema aliahidi kuwa ‘Mungu
akipenda’ atakuwa tena ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria Novemba
mwaka huu baada ya uchaguzi mkuu.
Kuondoka kwa mbunge huyo pia kunaifanya nafasi ya
uenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali(PAC) kuwa wazi kwa kuwa ndiye
aliyekuwa akiishikilia hadi alipotangaza rasmi juzi kuachia ubunge.
Akizungumzia uamuzi wa Zitto na juu ya mafao yake
baada ya kuamua kuondoka mwenyewe, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John
Joel alisema kuwa mbunge huyo atalipwa mafao yake yote.
“Unajua Chadema wametangaza kumvua uanachama Zitto
lakini hawajampa barua, sasa yeye ameona kuwa kuliko kuendelea na
ubunge wake ni vyema akakaa kando. Kutokana na suala hilo atalipwa tu
mafao yake yote,”alisema Joel.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wajumbe wa PAC
wamesikitishwa na kuondoka kwa Zitto kabla ya muda wa Bunge la 10
kumalizika huku wakimwelezea ni kiongozi aliyeweza kuwaunganisha katika
kamati bila kujali itikadi za vyama.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wajumbe hao
walisema aliwafanya wajumbe wa kamati hiyo kuwa familia na aliwaamini
na kuwaheshimu wote.
“Ni mtu aliyekuwa na ushirikiano na aliweza kutuunganisha bila kujali itikadi.
Alitufanya kama familia na alituamini na
kutuheshimu. Tunamtakia kila la kheri katika mipango yake ijayo,”alisema
Ismail Aden Rage (Tabora Mjini).
Mbunge wa Mkwamtipura, Kheir Ali Khamis alisema
kujiuzulu kwa Zitto ni suala la Kikatiba asingeweza kuendelea kushika
nafasi hiyo.
“Hili ni suala la Kikatiba haki ya kuwa mbunge inaondolewa ukishakuwa si mwanachama wa chama cha siasa,”alisema.
Alisema kutojiondoa mwenyewe kungeleta mgogoro kati yake na chama chake kwa kuwa tayari walishamvua uanachama.
Post a Comment