Serikali
imewasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na
dawa za kulevya ambao unawabana wauza ‘unga’ ukipendekeza kuwa
watakaobainika kufanya biashara hiyo haramu watozwe faini ya Sh. bilioni
moja au kifungo kisichopungua miaka 30, huku wabunge wakitaka
watakaobainika wapigwe risasi hadharani au wanyongwe.
Aidha,
atakayekutwa analima, kusambaza mbegu, kusafirisha, kuzalisha au
kuingiza mimea inayozalisha dawa za kulevya kama bangi, mirungi na
cocaine atatozwa faini isiyopungua Sh. milioni 20, kifungo kisichozidi
miaka 30 au vyote kwa pamoja.
Wakichangia
muswada huo ambao uliwasilishwa bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri MKuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenister Mhagama (pichani),
wabunge walipendekeza kufutwa kwa kipengele cha faini kwa kuwa
kinatengeneza mazingira ya rushwa kwa watendaji wa serikali wanaohusika
na kazi ya udhibiti wa dawa za kulevya, kwa kuwa wanaofanyabiashara hiyo
ni watu wenye mabilioni ya fedha.
Mbunge
wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, alisema vita dhidi ya dawa za kulevya
inakuwa ngumu kutokana na tabia ya serikali kulinda watuhumiwa hata pale
ushahidi unapokuwa wazi.
Alisema
ili kukomesha tabia hiyo, sheria hiyo inapaswa kutamka kwamba
watakaobainika kujihusisha na biashara hiyo adhabu ndogo iwe kifungo cha
maisha, kunyongwa hadi kufa au kupigwa risasi hadharani na kwamba
adhabu ya faini iondolewe.
“Bila
hivyo, tutakuwa tunabadilisha chupa, lakini mvinyo ni ule ule. Tatizo
tulilonalo ni kulindana siyo vyombo vya usimamizi. Polisi wakikamata
mfanyabiashara wa dawa hizi, simu za wakubwa zinapigwa wanawaachia, kwa
hiyo mimi sikubaliani na hili la kuanzisha mamlaka kama hatutaondoa
tatizo la kulindana,” alisema.
Alisema
wafanyabishara wa dawa za kulevya wanajulikana kwa majina hadi nyumba
wanazoishi lakini hawachukuliwi hatua badala yake vyombo vya dola
vinahangaika kukamata wasafirishaji wadogo wadogo.
Aidha,
alikiri kuwa na orodha ya majina na namba za nyumba wanakoishi
wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini, lakini hawezi kuwataja
bungeni hapo kutokana na hali ya sasa kuonyesha kuwa mfumo mzima
unawalinda wafanyabiashara hao.
Naye
mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, pamoja na kutaka
watakaokutwa na dawa za kulevya kunyongwa au kupigwa risasi hadharani
wiki mbili baada ya kuhukumiwa, pia aliitaka Serikali itafute mbinu ya
kuondoa dhana kuwa wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo wanalindwa.
Mbunge
wa Chambani (CUF), Yusuph Salim Hussein, aliungana na wenzake na kutaka
adhabu ya kifo cha kunyongwa au kupigwa risasi hadharani kwa
watakaojishughulisha na dawa za kulevya huku akisisitiza adhabu hiyo ni
stahiki kutokana na madhara makubwa ya dawa hizo kwa jamii.
“Lakini
pia naomba niulize inakuaje mtu anakutwa amemeza kete tumboni za dawa
za kulevya, anazitoa tumboni lakini hachukuliwi hatua eti kwa sababu ya
uchunguzi, uchunguzi gani? Watu kama hawa wahukumiwe palepale,” alisisitiza.
Mbunge
huyo alimtaja kijana mitano sasa, kwa kosa la kukutwa akisafirisha dawa
za kulevya, akisema tajiri aliyemtuma ambaye alimtaja kwa jina moja la
Dewji yuko nje na wala hajawahi kuhojiwa.
Mbunge
wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde, alisema ni wakati sasa
Serikali ianze kufanyia kazi hukumu za kunyongwa zinazotolewa na majaji
kwa watuhumiwa wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi au kukutwa na
kuuza dawa za kulevya ili kukomesha vitendo hivi.
“Sasa
hivi kuna kesi za wauaji wa albino zimetolewa hukumu ya kunyongwa,
lakini mpaka leo hawa watu hawajanyongwa, kwa sababu Rais hajasaini,
sasa tunapendeza kunyongwa pia hawa dawa za kulevya, Rais kabla
hajaondoka madarakani, asaini wanyongwe,” alisisitiza.
Alisema
serikali inapata kigugumizi cha kuwabana wafanyabiashara wa kubwa wa
biashara hiyo kwa kuwa ni matajiri wenye nguvu ya kufanya jambo lolote
kujilinda.
Awali,
akiwasilisha muswada huo, Mhagama alisema katika kuiongezea ukali
sheria hiyo, adhabu za watu wote watakaoukutwa, kutumia, kufadhili au
kufanya dawa za kulevya zimeongezwa na kuwa kali zaidi.
Serikali
inakusudia kuanzisha Chombo kinachojitegemea chenye mamlaka ya
kiutendaji ya kuchunguza, kupekua na kukamata watuhumiwa tofauti na
ilivyo Tume.
Nayo
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi, imeungana na wabunge
kwa kutaka adhabu ya faini iondolewe kwenye sheria hiyo badala yake
ibakie kifungo cha maisha au kunyongwa, pindi mtuhumiwa atakapothibitika
kuhusika na biashara hiyo.
Akiwasilisha
maoni ya kamati hiyo, mbunge wa Viti Maalum (CCM), Neema Himd, alisema
wakulima wa mimea ya dawa za kulevya kama bangi, kamati hiyo
imependekeza kuwa watakaobainika waongezewe kifungo na kusiwepo na
faini.
Alisema
Kamati pia imependekeza kuwa baadhi ya wadau wameeleza kuwa hivi sasa
wauza ‘unga’ wameanza kutengeneza wateja kwa kuweka dawa hizo kwenye
vyakula na vinywaji kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, hivyo
akapendekeza kuwa adhabu iwe kali ili kukomesha uharamia huo.
Naye
msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani katika Wizara hiyo, Rajab Mohamed
Mbarouk, alisema ili sheria hiyo iwe kali, lazima adhabu iwe ni kifungo
cha maisha au kunyongwa hadi kufa badala ya kuweka adhabu ya faini au
kifungo.
“Kambi
rasmi inapendekeza kufuta masharti yote yanayotoa nafasi ya kulipa
faini kwa mtu atakayepatikana na biashara ya dawa za kulevya na badala
yake kuacha masharti ya kifungo pekee, hii itasaidia kukomesha biashara
hii haramu ambayo inaangamiza nguvu kazi ya Taifa,” alisema.

Post a Comment