Dar/Dodoma. Licha ya Serikali kusisitiza kuwa
uandikishaji wa wapigakura nchi nzima kwa mfumo wa BVR utakamilika
Aprili 28 na Kura ya Maoni kufanyika Aprili 30, mwaka huu kama
ilivyopangwa, hesabu zilizopigwa na Mwananchi zinakataa kuwianisha siku
zilizosalia na idadi ya mashine za BVR zilizopo na zinazotarajiwa
kuwasili. Hali hiyo imejitokeza zikiwa zimebaki siku 36 kabla ya Kura ya
Maoni kufanyika, huku kukiwapo wasiwasi miongoni mwa wadau kuhusu
uwezekano wa kufanikisha matukio hayo bila manung’uniko.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwaeleza waandishi wa
habari jana kuwa uandikishaji nchi nzima utaanza siku sita kuanzia leo
na kusisitiza kuwa Kura ya Maoni kuridhia au kukaa Katiba
Inayopendekezwa itafanyika Aprili 30, mwaka huu kama ilivyopangwa.
Wasiwasi wa kutofanyika kwa kura hiyo katika
tarehe iliyopangwa unatokana na uandikishaji wa wapigakura kwa BVR
unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ulioanza Februari 23,
mwaka huu kutokamilika hata katika mkoa mmoja wa Njombe, wenye
wapigakura 392,634 kati ya milioni 24 wanaotarajiwa kuandikishwa nchini
kote.
Hesabu zinavyokataa
Kulingana na takwimu za NEC, BVR moja inaandikisha
kati ya wapigakura 80 hadi 100 kwa siku endapo hakuna tatizo lolote,
hivyo kwa kadirio la chini, iwapo BVR 7,750 zilizoagizwa na NEC
zitawasili nchini kwa mafungu, zitahitajika siku 38 kuandikisha
wapigakura milioni 24 wanaokusudiwa kama kazi hiyo itaanza leo.
Hata hivyo, katika uandikishaji wa majaribio na
baadaye katika Mkoa wa Njombe mashine hizo zimeripotiwa kukabiliwa na
changamoto mbalimbali ama za kukwama, weledi mdogo wa watumiaji na hali
ya hewa, hivyo kufanya idadi iliyokusudiwa kutokamilika.
Mwandishi wa Mwananchi, Kizzito Noya aliyekuwa
Makambako, Njombe wakati wa uandikishaji hivi karibuni amesema kwa
wastani alishuhudia mashine moja ya BVR ikiandikisha wapigakura 60 kwa
siku, idadi hiyo ikilinganishwa na watu 24,000,000 wanaokusudiwa
kuandikishwa kwa BVR 7,750 nchi nzima, shughuli hiyo itachukua siku 52,
wakati siku zilizosalia hadi Kura ya Maoni ni 36.
Jambo jingine linalofanya hesabu hizo kukataa ni
kitendo cha mashine hizo 7,750 za BVR zilizokusudiwa, kutokuwapo zote
nchini hadi sasa, licha ya NEC kusema mara kwa mara kwamba zitawasili
wakati wowote.
Jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema hata awamu ya kwanza ya mashine 3,100 za BVR bado ziko njiani.
Iwapo mashine hizo pekee zitafika na kutumika
kuandikisha wapigakura hao milioni 24 zitahitajika siku 97 kukamilisha
shughuli hiyo.
Mchakato huo ulianza kusuasua tangu wakati
majaribio yaliyotumia BVR 250 katika majimbo ya Kilombero, Morogoro;
Kawe, Dar es Salaam na Milele mkoani Katavi na baadaye katika Mji wa
Makambako na mkoa mzima wa Njombe.
Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa
mashine hizo 250 zimekuwa hazitumiki zote kwa kuwa baadhi zinatumika
kutoa mafunzo kwa waandikishaji watakaofanya kazi hiyo nchi nzima

Post a Comment