Hatimaye mbunge wa Monduli, Edward Lowassa amesema
“ameshawishika” na kuweka bayana kuwa atachukua fomu ya kugombea urais
kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya
Awamu ya Nne, amekuwa akitajwa kuwa ni mmoja wa makada wa CCM
wanaowania urais, lakini hakuwahi kutangaza nia ya kuwania nafasi hiyo
ya juu ya uongozi nchini.
Lakini jana, alilazimika kufunguka kuhusu suala la
urais ambalo lilimfanya yeye na wenzake watano wafungiwe kwa kipindi
cha miezi 12 kujihusisha na harakati hizo baada ya Kamati Kuu ya CCM
kuwatia hatiani kuwa walianza kampeni mapema kabla ya muda kufika.
“Nimepata barua za ushawishi kutoka kwa watu
wengi, lakini nyinyi nimeshawishika,” alisema Lowassa nyumbani kwake
mjini Dodoma wakati alipokuwa anazungumza na masheikh wa misikiti ya
Wilaya ya Bagamoyo wanaokadiriwa kuwa kama 50 hivi ambao pia walikuja
mjini hapa kwa ajili ya kumshawishi aingie kwenye kinyang’anyiro cha
urais na kumkabidhi mchango wa Sh700,000 za kuchukulia fomu.
“Lakini bado kuna taratibu za chama za kuheshimu. Nangojea pale watakaposema sasa tuwe, basi itakuwa.”
Lowassa alifungiwa na CCM Februari 18, 2014 pamoja
na Bernard Membe, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Steven Wasira (Kilimo, Chakula na Ushirika), na January
Makamba (Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia).
Wengine waliofungiwa ni Frederick Sumaye, ambaye
alikuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu na William Ngeleja
(Mbunge wa Sengerema).
Pamoja na adhabu hiyo kumalizika Februari 18, CCM
imesema Kamati ya Maadili inaendelea na uchunguzi kwa ajili ya
kujiridhisha kama miongoni mwao kuna waliokiuka adhabu hiyo kabla ya
kuwasilisha mapendekezo kwenye Kamati Kuu ambayo itafanya uamuzi.
Masheikh waliofika jana nyumbani kwake wanatoka
maeneo ya Mlingotini, Kondo, Kaole, mjini Bagamoyo, Lugoba na Chalinze
wilayani Bagamoyo.
Mbali na kumuomba atangaze nia, masheikh hao pia walimsomea dua ya kumtakia heri katika harakati hizo.
“Nyie ni special (maalum), mnatoka Bagamoyo na
inajulikana kwa historia na ni nyumbani kwa Rais (Jakaya Kikwete).
Namimi nimepata baraka zake na nyie mmemuwakilisha,” alisema Lowassa.
“Tumetoka naye mbali sana, lakini Mwenyezi Mungu
akinijalia nitaanzia pale alikomalizia. Amefanya kazi kubwa na ya
heshima kwa kweli. Kwa hiyo kitendo cha kutoka nyumbani kwenu kuja
kuniona kwa kweli kimenipa nguvu kwamba wenzangu wa Bagamoyo wako pamoja
na mimi.”(Mwananchi)
Post a Comment