JAMBO limezua jambo! Siku chache
baada staa wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ kudaiwa
kumfumania mpenzi wake Siwema Edson kisha kuondoka na mtoto wa miezi
mitatu (Curtis), mrembo huyo ameibuka na kudai mtoto huyo si mali ya
Mbongo Fleva huyo hali ambayo imesababisha mama yake mzazi Nay apate
mshtuko, Ijumaa Wikienda linakupa mchapo hatua kwa hatua.
Nay wa Mitego na Siwema wakiwa na mtoto wao anayejulikana kwa jina la Curtis.
SAKATA LILIVYOANZA
Ijumaa
iliyopita, gazeti tumbo moja na hili la Ijumaa liliripoti tukio la Nay
kutonywa kuwa mchumba’ke anachepuka jijini Mwanza anakoishi ambapo Nay
aliamua kufunga safari kutoka Dar hadi Mwanza na kumfumania Siwema akiwa
na ‘serengeti boy’ wake.
HABARI YAMTIBUA SIWEMA
Mara baada ya habari hiyo kupeperuka hewani, rafiki wa karibu na
Siwema alimvutia waya mwanahabari wetu ambapo alieleza jinsi gani Siwema
amechukizwa na habari hiyo.
TUJIUNGE NA SHOSTI
“Nilikuwa na Siwema, kusema kweli amemlalamikia sana Nay, anasema
tangu alipokuwa mjamzito alikuwa na mgogoro mkubwa sana na Nay, hata
alipojifungua amekuwa akivumilia vitu kibao kutoka kwa jamaa (Nay)
Mbongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ akiwa na mpenzi wake Siwema.
ETI HALIKUWA FUMANIZI
“Zaidi alichokuwa akilalamikia Siwema ni juu ya Nay kusema
alimfumania wakati siku hiyo yeye alimkuta anamnyonyesha mwanaye, hata
anaposema kamkuta na mwanaume, haoni hoja ya Nay kusema hilo wakati
mwenyewe alimwambia hamtaki na kumruhusu kutafuta bwana sasa amemkuta
analalamika nini tena?
KIGOGO AMPA JEURI SIWEMA
“Kwanza Siwema ana kigogo wake serikalini ndiye anayempa jeuri, sasa sijui hata anamfuatafuata wa nini,” alisema rafiki huyo.
SIWEMA ANASEMAJE?
Baada ya kunasa mazungumzo hayo ya shosti huyo, mwanahabari wetu
alimsaka Siwema mwenyewe ili kujua anazungumziaje sakata hilo,
alipopatikana, alifunguka:
“Yaani we acha tu katika maisha huwa kuna siri sana, najua watu wengi
wanaongea mambo ambayo hawayajui vizuri, nimeanza uhusiano na Nay siku
nyingi sana na kote huko mimi mambo yangu yalikuwa safi kuliko yeye
ambaye hata jina alikuwa hana, namshangaa sana leo maneno anayoropoka
kwa watu eti alinifumania wakati siku anakuja kwangu alinikuta nimembeba
mwanangu Curtis na nilikuwa namnyonyesha, nafikiri ajaribu kumuogopa
Mungu kidogo.
AZIDI KUFICHUA MAOVU
“Kuna uchafu mwingi sana alikuwa akinifanyia na hata hivyo kusema
kanihonga gari, ni muongo kwani hili gari (Toyota Mark X) ni langu,
hakumbuki zile Toyota Lexus na Toyota Verossa zangu nilizompa?
Amenirudisha nyuma sana kimaisha hata mama na dada yake anajua haya,
tangu nimekuwa naye mimi ndiyo mkosaji tu? Mimi huyuhuyu ndiye nilikuwa
nikimuomba msamaha kila kukicha hadi mwisho akanitamkia nitafute
boyfriend, hata hilo bado hakumbuki na kuendelea kuongea vya uongo?”
APIGILIA MSUMARI WA MTOTO
“Najua kweli ana watoto zaidi ya watatu nafikiri hata hao wengi bado
ana muda wa kuwataja tu na wajulikane kwenye jamii asijifanye anampenda
sana Curtis, amuache tu maana si wake mimi ndiye ninayeweza kujua zaidi
baba wa mtoto na asijifanye kimbelembele na kutaka kunichafulia kwenye
jamii wakati ukweli naujua mimi,” alisema Siwema.
MAMA APATA MSHTUKO
Kufuatia habari hiyo ya Nay kumfumania Siwema na mchumba huyo wa
mwanaye kufunguka kuwa mtoto si wa Nay, chanzo kilicho karibu na familia
ya msaanii huyo kimepenyeza habari kuwa mama mzazi wa Nay, Matlida
Mwaipopo alipata mshtuko na kushindwa kuzungumzia suala hilo.
“Mama Nay amepata mshtuko mkubwa, presha imepanda na hapa
tunavyoongea na wewe, tumejaribu kumtuliza ili aweze kusaidia tatizo
hili kifamilia, ameshindwa kuzungumzia lolote,” kilisema chanzo hicho.
NAY ALIA USIKU KUCHA
Alipotafutwa Nay kuhusina na tukio hilo, alishindwa kuzungumzia
lolote zaidi ya kulia kutwa na hata alipotafutwa baadaye bado
alizungumza huku akilia.
Gari aina ya Toyota Lexus aliyonunuliwa Siwema na Nay.
“Suala la kuambiwa mtoto si wangu linaliza na hadi muda huu naumia
sana, inafikia wakati nashindwa hata niseme nini ila anachokitaka kwangu
atakipata, wewe mwacheni aendelee kuropoka na kunidhalilisha huko
Instagram, ukweli mimi sina neno naye na zaidi nimechukua mtoto wangu na
nawapenda sana wanagu wote,” alisema Nay na hata alipotafutwa usiku
sana siku hiyo (Ijumaa iliyopita), bado alisikika akilia kwa uchungu.
KIKAO CHA FAMILIA CHAANDALIWA
Wakati gazeti hili linakwenda mitamboni, chanzo makini kilivujisha
habari kuwa kuna baadhi ya ndugu wa karibu wa Nay wanaandaa kikao cha
familia ili kutafuta suluhu ya jambo hilo.
“Kuna kikao kizito kinaandaliwa cha familia kutafuta suluhu lakini tutakujuza zaidi kitakapofanyika,” kilisema chanzo hicho
Post a Comment