Na. Johary Kachwamba-MAELEZO, DODOMA
SERIKALI
imeweza kushawishi mashirika ya kimataifa ya ndege kuongeza idadi ya
safari pamoja na kiwango cha mzigo kinachosafirishwa kutoka Tanzania
kwenda nje ya nchi, ikiwemo bidhaa za matunda.
Naibu
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Janet Mbene (pichani) alibainisha
hayo bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Muhammad Sanya,
Mbunge wa Mji Mkongwe aliyehoji mpango wa Serikali katika kutafuta soko
la matunda nje ya nchi.
Mhe.
Mbene alisema TanTrade kwa kushirikiana na Chama cha Wazalishaji Maembe
(AMAGRO) inaratibu mpango wa kutoa mafunzo ya uzalishaji bora,
ufungashaji na kujenga kituo cha kuchambua na kupanga ubora wa maembe
ili kuuzwa kwenye soko la kimataifa.
Aidha kampuni ya AMAGRO inaendelea kuhamasisha kilimo cha maembe aina ya tommy na alphonso ili kuuza soko la nje.
“mkoani
Tanga tumeanzisha program ya Muunganisho wa Ujasiriamali Vijijini
(MUVI) katika vijiji 9 ili kuzalisha machungwa yasiyo mbegu kwa matumizi
ya ndani na soko la nje ” alisema Mhe. Mbene
Tayari
kampuni ya Africado inayozalisha maparachichi Wilayani Hai na Kampuni
ya Rungwe Avocado ambapo yote yanawakilisha wakulima wadogo,
yanazalisha na kuuza maparachichi soko la nje ya nchi.
Aidha
Mhe. Mbene alisema Serikali imeanzisha kampuni ya GS1 Tanzania
inayoratibu mfumo wa ufuatiliaji wa mnyororo wa bidhaa ambao ni msingi
mkubwa katika kupata soko la bidhaa yoyote nje ya nchi.
“Serikali
inaendelea kutangaza bidhaa za Tanzania kupitia maonesho ya Biashara ya
ndani, kikanda na kimataifa” aliongezea Mhe. Mbene
Mkakati
wa Mauzo ya Nje (National Export Strategy) wa Mwaka 2009 ulibainisha
mikakati ya kuongeza mauzo ya matunda, maua na mbogamboga. Kutokana na
hali hii thamani ya mauzo ya matunda nje imeongezeka kutoka Dola za
kimarekani 7,440,290 mwaka 2010 hadi Dola za kimarekani 32,116,895.22
mwaka 2013.

Post a Comment