Wadau wa uchumi
Ujumbe
wa nchi za umoja wa ulaya umekutana jijini Dar es salaam Tanzania
kujadiliana na wenzao wa afrika mashariki juu ya mkataba wa ushirikiano
wa kiuchumi unaofahamika kama EPA unaotegemewa kutiwa saini baadae mwaka
huu.
Hata hivyo ushirikiano huo unaleta wasiwasi kwa baadhi ya wadau iwapo nchi za afrika mashariki zitafaidika na ushirikiano huo.
Kutoka Dar es salaam mwanahabari wetu Arnold Kayanda amehudhuria mkutano huo na hii ni taarifa yake.
Mkutano
huo wenye lengo la kujadili na kufanyia kazi makubaliano yaliyomo
katika mkataba wa EPA umewakutanisha wawakilishi wa umoja wa nchi za
ulaya na wadau wakiwamo wafanyabiashara wakubwa wa Tanzania. Miongoni
mwa wafanyabiashara wa Tanzania waliohudhuria mkutano huo ni Ali Mfuruki
ambaye hadhani kama ushirikiano huu utazifaidisha nchi za Afrika
Mashariki kwa kuwa haziko tayari na ni bahati mbaya hatua iliyofikiwa
hairuhusu kurudi nyuma maana makubaliano ya msingi yameshafanyika.
“Afrika
mashariki na afrika kwa ujumla haitaweza tena kuunda msingi wa viwanda
katika uchumi, baada ya muda si mrefu tutakuwa tunakula mayai ya ulaya,
tunakunywa maziwa ya ulaya, tunakula kuku wa ulaya. Kwa sababu wenzetu
wamejitayarisha miaka mingi sana wako tayari kufanya biashara kuliko
sisi. Na sisi tumejiingiza katika hii mikataba bila kufanya matayarisho
,nina wasiwasi hata waliokuwa wanashiriki katika haya makubaliano
hawakufikiria mambo haya kwa upana na undani unaotakiwa” anasema Mfuruki
.
Athanassios Rammos ni afisa wa umoja wa ulaya anayehusika na
nchi za afrika mashariki katika masuala ya biashara anasema utayari
utakuja polepole wakati wa ushirikiano huo ukiwa umeanza kwa kuwa suala
la utayari si la siku moja.
“Kutakuwa na kipindi cha mpito ambacho
kitatoa muda wa kutosha kwa wazalishaji kujiandaa. Na hata hivyo ndani
ya mkataba tunatoa nafasi kwa nchi za afrika mashariki kusema wakati
wowote wanapoona kuna kitu hakiendi vizuri katika makubaliano”
Athanassios anasisitiza.
Mazungumzo ya kufikia makubaliano ya
ushirikiano huo wa kibiashara yalianza mwaka uliopita ambapo vikao
kadhaa vilifanyika bila kufikia muafaka mpaka mwaka ulipita ndipo
wakakubaliana. Hivi sasa wako katika hatua za mwisho za kuipitia vema
lugha ya mkataba na makubaliano yatakapopitishwa baadhi ya bidhaa za
afrika mashariki zitaondolewa vikwazo kuingia katika nchi za umoja wa
ulaya.
Takwimu za biashara za mwaka 2013 kati ya nchi za afrika
mashariki na nchi za umoja wa ulaya zinaonyesha nchi za umoja wa
ziliingiza afrika mashariki euro bilioni 2.2 kwa kununua bidhaa
mbalimbali hususani kahawa, maua, chai, tumbaku, samaki na mbogamboga
ilhali nchi za afrika mashariki ziliziingizia nchi za umoja wa ulaya
bilioni 3.5 za euro kwa kununua bidhaa kama vile mitambo, vipuri, magari
na dawa.(BBC)

Post a Comment