“NIMEPONEA CHUPUCHUPU KUKATWA MGUUU”

Brown Mwirwa (42), mkazi wa Tunduma wilayani Momba, Mkoa wa Mbeya  ameponea chupuchupu kukatwa mguu wa kulia uliovunjika mara mbili katika ajali ya kugongwa na gari hivi karibuni akiwa abiria kwenye pikipiki.Akizungumza na waandishi wetu katika Hospitali ya Upasuaji wa Mifupa na Viungo Burere iliyopo Kibaha Kwamathias, Pwani alisema ajali hiyo aliipata hivi karibuni akiwa abiria katika pikipiki.
Muonekano wa mguu wa Brown Mwirwa baada kugongwa na gari hivi karibuni akiwa abiria kwenye pikipiki.
AJALI ILIVYOTOKEA
Aidha, aliendelea kusema kwamba walikuwa wakipishana na gari dogo ambalo lilijaribu kuwapita, ghafla likakwepa gari lililokuwa linatoka mbele yao na kuwagonga.
KUZIMIA
Aliendelea kusimulia: “Nilizimia, sikujua kilichoendelea kwa muda huo, nilikuja kupata fahamu nikiwa polisi tunachukua hati namba tatu ya polisi (PF3) ya matibabu nikapelekwa Zahanati ya Tunduma ambapo madaktari wakasema hawawezi kunitibu, nikahamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Mbozi.“Hapo walinipima wakasema tiba imeshindikana kwani madaktari waligundua kuwa nimevunjika mguu mara mbili.”
KUHAMISHIWA HOSPITALI YA RUFAA
“Nilihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, madaktari wakasema mguu wangu umevunjika vibaya sana hivyo niletwe Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu  Muhimbili (MOI) ambako kuna wataalam.
“Hata hivyo, ndugu zangu walikaa na kujadili baadaye wakaamua wanilete hapa Kibaha kwa Dk. Bake Burere.”
Brown Mwirwa akiwa amejilaza hospitalini.
NILIAMINI MGUU UTAKATWA
“Mara nilipofika hapa nilifanyiwa uchunguzi na Dk. Bake, niliamini kwamba mguu wangu utakatwa kwa kuwa ulikuwa umevunjikavunjika vibaya lakini namshukuru Mungu nikaambiwa na daktari kwamba hauwezi ukakatwa.
 “Alisema hautakatwa kwa sababu nimeuwahisha kuuleta hapa hospitali kabla ya kuoza na kwa sasa naendelea vizuri.”
SHILINGI LAKI TANO ZAHITAJIKA
“Dokta amenihakikishia kuwa nitapona na nitaendelea na shughuli zangu kama kawaida. Kwa sasa nimepata nafuu kwa kiasi kikubwa, nawashukuru ndugu, jamaa na marafiki kwa kunichangia fedha ya kunifikisha hapa ila bado zinahitajika zaidi ya shilingi laki tano za matibabu.
“Nawaomba Watanzania wanisaidie katika matibabu.
...Akipatiwa matibabu.
“Nipo katika mtihani mgumu kutokana na ugonjwa huu na najua familia yangu kwa sasa inateseka kutokana  na ukweli kwamba mimi ndiyo nilikuwa msaada mkubwa kwao kwa kila kitu.“Namshukuru Dk. Bake na manesi, wameokoa mguu wangu kwani sasa nina hakika hautakatwa. Mungu awabariki sana.“Kwa yeyote ambaye ataguswa na matatizo yangu anaweza kuwasiliana nami kwa namba 0759 503235 au 0757 481624.”

Post a Comment

Previous Post Next Post