Utekelezaji
wa adhabu ya kifo kwa watu 10 waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa,
kutokana na kuhusika katika mauaji ya watu wenye ulemavu (albino),
unasubiri saini ya Rais Jakaya Kikwete.
Hayo
yalibainishwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame
Silima, wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Lindi Mjini, Salum
Barwany (CUF).
Katika
swali lake, Barwany, alitaka kufahamu ni lini utekelezaji wa hukumu ya
kifo kwa watu 10, waliokwisha hukumiwa adhabu ya kifo na Mahakama
kutokana na kuhusika na mauaji ya albino, itatekelezwa.
Silima, alisema kwa mujibu wa taratibu za kisheria, adhabu ya kifo inapotolewa, utekelezaji wake husubiri saini ya Rais. “Sijapata
taarifa kama hukumu hizi tayari Rais ameziwekea saini ili zitekelezwe
ila nitafuatilia ili Sheria ichukue mkondo wake,” alisema.
Katika
swali la msingi la mbunge huyo, alitaka kufahamu hadi sasa kuna kesi
ngapi za mauaji ya walemavu wa ngozi zilizokwishatolewa hukumu baada ya
kufikishwa mahakamani na kesi ngapi bado zinasubiri huku na ni kwanini
zimechelewa kutolewa maamuzi.
Waziri
alisema kati ya mwaka 2006 na 2015, jumla ya matukio 56 ya uhalifu
dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi yaliripotiwa nchini na kati ya
matukio hayo 41 yalihusisha vifo 43, matukio 13 yahusisha majeruhi na
mawili ya kupotea watu hao albino.
Alisema
kesi 46 kati ya matukio 56 zilifikishwa mahakamani na kesi 10 zenye
watuhumiwa 12 zilitolewa hukumu ya kifo na kesi 10 badi ziko chini ya
upelelezi. Aidha kesi 26 watuhumiwa wake waliachiwa huru kwa kukosa
ushahidi.
Silima alisema pia kesi 10 bado zinaendelea kusikilizwa mahakamani na ziko katika hatua mbalimbali.
“Kuhusu
kuchelewa kwa hukumu au upelelezi wa baadhi ya kesi, kunachangiwa na
sababu mbalimbali kama vile matokeo ya uchunguzi wa vinasaba (DNA)
kutoka mamlaka za uchunguzi na mashahidi kutopatikana kwa urahisi na
wakati".
Katika
swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalum, Al- Shamaar Kwegyir (CCM),
alitaka kujua Serikali imefikia wapi katika kumtafuta mtoto Pendo
Emmanuel mwenye ulemavu wa ngozi mkazi wa Kwimba, aliyechukuliwa
mikononi mwa mama yake mzazi na mpaka sasa hajulikani alipo.
Akijibu
swali hilo, Silima alikiri kuwa mpaka sasa Polisi inamtafuta na katika
upelelezi unaoendelea jumla ya watu 14 wanashikiliwa na kuhojiwa kwa
kuhusika kwa namna moja ama nyingine na tukio hilo, akiwemo baba mzazi
wa mtoto huyo.
“Pendo
alichukuliwa mikononi mwa mama yake, na hali hii ndio inayoongeza ugumu
wa matukio haya kwa Serikali kuyapatia ufumbuzi, jambo la msingi
tusiwaachie polisi pekee, jamii nayo ijihusishe kuwalinda na kuwaripoti
wahusika,” alisema.
Alisema
hata yeye matukio hayo yanamtoa machozi kwa kuwa inaonesha sasa
Watanzania wameondokewa na utu wa ubinadamu, na ndio maana wanafanya
ukatili na unyanyapaa dhidi ya jamii ya albino.
Post a Comment