Vyombo vya habari jana viliandika kuhusu mahojiano baina ya
Sekretarieti ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma na viongozi wawili
wa umma, Andrew Chenge na Profesa Anna Tibaijuka ambao wametuhumiwa
kukiuka maadili katika sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya
Tegeta Escrow.
Chenge alifikishwa mbele ya chombo hicho
akituhumiwa kutumia nafasi yake ya zamani ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali kujinufaisha na mkataba wa kuzalisha umeme kati ya Serikali na
kampuni binafsi ya IPTL ambayo inaliuzia nishati Shirika la Umeme
(Tanesco).
Profesa Tibaijuka anatuhumiwa kukiuka maadili kwa
kuingiziwa Sh1.6 bilioni kwenye akaunti yake akiwa kiongozi wa umma
tofauti na masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Chenge
alizuia shauri lake lisijadiliwe baada ya kuomba Mahakama Kuu itoe
tafsiri ya zuio la mahakama dhidi ya vyombo vya Serikali kujadili kashfa
ya escrow.
Hata hivyo shauri la Profesa Tibaijuka
lilijadiliwa na sasa, kwa mujibu wa taratibu litawasilisishwa kwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano kwa hatua zaidi.
Kilichoshangaza na kuwaacha wengi midomo wazi ni
jinsi Tibaijuka, mbunge wa Muleba Kusini, alivyojitetea kuhusu matumizi
ya Sh10 milioni alizochukua kutoka kwenye akaunti yake baada ya
kuingiziwa na mmiliki wa zamani wa Kampuni ya IPTL, James Rugemalira.
Alipoulizwa sababu za kuchota fedha hizo kwenye akaunti wakati anadai
aliziomba kwa ajili ya shule yake, waziri huyo wa zamani wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi alijibu kuwa fedha alizotoa zilikuwa ni
kwa ajili ya “kununua mboga”.
Mkurugenzi huyo wa zamani wa Shirika la Makazi la
Umoja wa Mataifa (UNHabitat) anaweza kutoa maelezo mengi kufafanua suala
hilo, lakini hayataweza kufuta dhana kuwa amefikia kiwango cha juu cha
kebehi kwa Watanzania wengi ambao kwa viwango vya kimataifa, hata
UNhabitat, wanaishi chini ya Dola 1 ya Marekani (yaani Sh1,820 za
Tanzania). Kwa taifa ambalo asilimia 36 ya wananchi wake wanaishi chini
ya hali ya umaskini, kauli hiyo siyo mzaha kwa wajumbe wa Sekretarieti
ya Maadili, bali ni shambulio kubwa kwa wananchi ambao wamekata tama ya
maisha, kwa vijana ambao wanashindia pombe kali za kwenye pakti
kujisahaulisha machungu ya maisha; kwa wakulima ambao wanalazimika kula
mizizi kutokana na njaa; kwa wafanyakazi ambao mishahara yao haitoshi
kupanda magari wawahi kazini na kulazimika kutembea umbali mrefu kufuata
kibarua pia wanafunzi wanaokosa mikopo kujiendeleza na masomo ya juu.
Hawa wote wanaposikia kiongozi wa umma anachukua
Sh10 milioni kwa ajili ya mboga, wanakata tamaa ya maisha zaidi kiasi
kwamba huwezi tena kuwaambia wafanye kazi kwa bidii ili wapate mafanikio
wakati wanajua wako wanaotumia kiasi kikubwa cha fedha kununulia mboga.
Profesa Tibaijuka siyo kiongozi pekee wa umma
ambaye amewahi kutoa maneno kama hayo wakati akiwa akikabiliwa na tuhuma
nzito. Akiwa anakabiliwa na tuhuma za kuhusika kwenye sakata la ununuzi
wa rada kwa bei ambayo inaumiza uchumi wa nchi na taarifa kuwa aliweka
Sh1.8 bilioni kwenye akaunti yake nje ya nchi, fedha zilizohusishwa na
kashfa hiyo, Chenge alijibu kirahisi kuwa pesa hizo ni “vijisenti tu”.
Mapato ya viongozi wa umma yanajulikana na iwapo
walipata kabla ya kuingia madarakani, wanatakiwa watangaze na kuboresha
taarifa za mali zao kila wanapopata zaidi. Inapotokea vyombo
vinavyowakilisha wananchi vinahoji kuhusu ongezeko la ghafla la mali, ni
vizuri wakatoa maelezo yasiyokera na yasiyoongeza hasira kwa wananchi
maskini.
Post a Comment