Jengo
la zahanati ya kijiji cha Lamba kata ya Mgori jimbo la Singida
kaskazini ambalo inadaiwa limekamilika kujengwa zaidi ya miaka mitatu
lakini hadi sasa halijaanza kutumika. Kitendo cha kushindwa kuanza
kutumika kwa zahanati hiyo, inadaiwa kusababisha usumbufu wakazi wa
kijiji cha Lamba kufuata huduma za afya kwenye kijiji cha Ngimu kilometa
15 au kijiji cha Mgori kilometa nane.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu, Singida
WAKAZI
wa kijiji cha Lamba kata ya Mgori jimbo la Singida kaskazini,juzi
walizuia/walisimamisha msafara wa mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko
Kone kuendelea na safari ya kikazi, kama njia ya kumshinikiza ili aweze
kusikiliza kilio chao juu ya huduma ya afya.
Wakazi
hao wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 30,walisimamisha msafara huo uliokuwa
ukielekea katika hifadhi ya msitu wa Mgori kwa ajili ya kuadhimisha siku
ya kitaifa ya utundikaji wa mizinga ngazi ya mkoa.
Baada
ya msafara huo kusimama,wakazi hao walimweleza Dk.Kone kuwa toka
zahanati ya kijiji chao imalizike kujengwa miaka mitatu iliyopita,hadi
sasa haijaanza kutoa huduma za afya.
Walidai
kitendo hicho kinaendelea kuchangia waendelee kupata usumbufu mkubwa wa
kufuata huduma umbali wa kilometa nane katika kijiji cha Mgori au
kilometa 15 hadi kijiji cha Ngimu.
“Mkuu
wetu wa mkoa, hatujakusimamisha ili tukupotezee muda wa kuendelea na
kazi zako za kuwahudumia wananchi, lengo letu ni kutaka utumie uwezo na
nguvu zako kututafutia ufumbuzi wa kudumu kuhusu tatizo la kushindikana
utoaji wa hudumu za afya kwa kipindi chote hichi cha miaka mitatu toka
kumalizika kwa ujenzi wa zahanati.
Akadai waathirika wakubwa na kasoro hii,ni akina mama wajawazito”,alisema mkazi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe humu.
Baada
ya kumaliza kukagua jengo la zahanati na jengo linaloendelea la nyumba
ya mtumishi wa zahanati hiyo ambalo lina miaka miwili toka lifikie hatua
ya lenta,Dk.Kone aliwapongeza wakazi hao kwa ujasiri wao wa kusimamisha
msafara na kuda kwamba wana haki ya msingi kusimamisha msafara wake.
Kwa
kifupi mkuu huyo wa mkoa,alisema kwamba zahanati hiyo kushindwa kuanza
kutoa huduma,ni udhaifu tu wa watendaji na kwamba kuanzia sasa
atashughulikia mapema iwezekanavyo kilio chao.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Singida,bwana
Mtefu,alijitetea kuwa muda mrefu halmashauri hiyo ina upungufu mkubwa wa
rasilimali fedha kitendo ambcho kimekuwa kikwazo kikubwa kwa ustawi wa
maendeleo ya halmashauri hiyo.
Habari
nyingine kutoka kwa kiongozi mwingine wa ngazi ya juu katika halmahauri
hiyo ambaye ametaka jina lake lisitajwe kwa madai kuwa sio msemaji wa
halmashauri hiyo, amedai kuwa zahanati hiyo haijakamilika kwa aslimia
mia moja kutokana na fedha karibu zote kuhamishiwa katika ujenzi wa
maabara.

Post a Comment