Dar es Salaam. Waziri wa
Uchukuzi, Samuel Sitta amezuia uingizaji wa mabehewa 124 ya mizigo
yaliyobaki katika zabuni iliyofanywa na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL),
hadi pale uchunguzi wa tuhuma za ufisadi katika manunuzi hayo
utakapokamilika.
Pamoja na hayo, Sitta alisema kuna hisia zimejitokeza kuwa huenda mabehewa hayo ni mitumba siyo mapya kama inavyodhaniwa.
Sitta aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa
zabuni ilihusisha ununuzi wa mabehewa 274 na kwamba 150 tayari
yalishaingia nchini, huku kukiwa na harufu ya ufisadi kuwa
yalitengenezwa chini ya kiwango.
Mapema Aprili 2013, TRL iliipatia kampuni ya India
iitwayo M/S Hindustan Engineering & Industrial Limited zabuni ya
kutengenezea mabehewa ya mizigo kwa ajili ya Reli ya Kati. Serikali
iliilipa kampuni hiyo Sh45.5 bilioni sawa na Sh166 milioni kwa kila
behewa.
Hata hivyo, Sitta alisema kuwa Serikali ililipa
asilimia 50 ya gharama zote za manunuzi na kwamba iwapo ikibainika
udanganyifu wowote kampuni hiyo itawajibika.
“Nimekataza kabisa yale 124 yaliyobaki kule
yasije. Nimeshawaagiza Reli kuwa yaliyopo kiwandani yanaendelea
kutengenezwa au safarini hayaruhusiwi kuja kwa sasa mpaka tuweze
kukwamua sakata hili.”
“Haiwezekani wakati tunachunguza 150 yaliyoingia
tukayaruhusu yale 124 yaingie. Je, yakiwa na ubovu ule ule itakuwaje?”
alihoji Sitta.
Alisema anaungana na aliyekuwa waziri wa wizara
hiyo, Dk Harrison Mwakyembe kuwa mabehewa hayo ya mizigo yapo chini ya
kiwango kutokana na kupinduka na kuacha reli mara kwa mara.
Alisema kiwango cha kuacha reli kwa mabehewa hayo
siyo cha kawaida na ripoti ya Desemba mwaka jana ilionyesha kulikuwa na
wastani wa upindukaji kila siku.
Kutokana na suala hilo kuwa kikwazo cha ufanisi
kwa TRL, Sitta aliiagiza kamati ya uchunguzi wa sakata hilo (iliyoundwa
na Dk Mwakyembe) kupitia Bodi ya Wakurugenzi ya TRL kukamilisha ripoti
ifikapo Ijumaa wiki hii ili Serikali ijue la kufanya.
“Kuna mambo mengi tu ya kufanya kama kuvunja
mkataba na mkandarasi, kumshtaki mhusika, kuangalia nani walienda
kukagua na bado tukapata vibovu.
“Hii itatusaidia kujua hatua za kuchukua
kiuwajibikaji kwa kuwa hivi sasa ni lazima mtu awajibike aidha kwa
kufanya jambo kwa makusudi au kwa uzembe,”alisema Sitta. Alisema Idara
ya Uhandisi katika wizara yake itasaidia kubaini nini kilitokea kiasi
cha kuingiza nchini mabehewa yanayoleta hasara kubwa kwa taifa.
Post a Comment