Yanga yamnasa straika kiboko ya Simba

Straika wa Mgambo JKT ya jijini Tanga, Malimi Busungu.
Na Sweetbert Lukonge,Dar es Salaam
AMA kweli Yanga imeamua, haitaki masihara kabisa. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya uongozi wa klabu hiyo kumwagia mamilioni ya fedha, straika wa Mgambo JKT ya jijini Tanga, Malimi Busungu.Yanga ambayo kwa muda mrefu ilikuwa ikiwinda saini ya mchezaji huyo, hatimaye imefanikiwa kuipata lakini kwa kutumia shilingi milioni 24.
Busungu hakamatiki kwa ufungaji, tayari msimu huu ana mabao sita na amekuwa akizitesa Simba na Yanga kila zinapokabiliana naye. Anakumbukwa zaidi kwa kuipiga Simba bao la pili wakati Msimbazi walipopokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Mgambo, Machi 18, kilichowaondolea matumaini ya kutwaa ubingwa Bara.
 Yanga inamchukua nyota huyo kama mchezaji huru kwa kuwa anamaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu.
Imeamua kumnasa mapema kwa kuwa inahofiwa atawahiwa kutokana na kuwa mchezaji huru lakini pia Yanga inajua kuwa amekuwa akiisumbua Simba mara kwa mara, hivyo huenda kutua kwake kutakomesha uteja kwa Wanamsimbazi. Kwa siku za hivi karibuni, Yanga imeshindwa kabisa kuibuka na ushindi dhidi ya Simba.
Habari za kuamini kautoka ndani ya Yanga zimedai kuwa, kamati ya usajili ya klabu hiyo kupitia kwa mwenyekiti wake, Isaac Chanji, tayari imemalizana na mchezaji huyo na atajiunga kikosi cha timu hiyo baada ya msimu kuisha.
“Tunamshukuru Mungu kwa kufanikisha mpango wetu wa kumsajili Busungu, hivyo msimu ujao tutakuwa naye katika kikosi chetu.“Tumemsajili kwa milioni 24 lakini pia tutampatia gari na nyumba ya kuishi kwa kipindi chote atakachokuwa na klabu yetu.
“Kuhusu mshahara, tumekubaliana naye kuwa atakuwa anachuka milioni mbili kwa mwezi katika kipindi cha miaka mitatu ya mkataba wake,” kilisema chanzo hicho cha habari.Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Yanga,  Dk Jonas Tiboroha, alipoulizwa juu ya suala hilo, hakuwa tayari kulizungumzia lakini alidai kuwa walikuwa na mpango wa kumsajili mchezaji huyo.
Alipotafutwa Busungu hakuwa tayari kuzungumza, akampa simu meneja wake ambaye kwa masharti ya kutotajwa jina alisema kweli Yanga wamemalizana na staa huyo wa maafande wa Mgambo.“Lakini bado hajasaini mkataba, atasaini Jumanne (kesho), kuhusiana na mshahara, fedha za usajili, nyumba na gari ni hivyohivyo kama ulivyoambiwa,” alisema meneja huyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post