Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima jana
alihubiri akiwa katika kiti cha magurudumu na kusema hawezi kuwatupa
Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willibrod Slaa kwa kuwa ni marafiki zake wa siku nyingi.
Pia askofu huyo, amewataka waumini wote wa kanisa
hilo kufika katika Kituo Kikuu cha Polisi, Alhamisi ijayo siku ambayo
atakwenda kukamilisha mahojiano dhidi ya tuhuma za kumtukana Askofu Mkuu
wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo.
Akihubiri mamia ya waumini waliofika kanisani hapo
kwa ajili ya ibada ya Pasaka jana, Gwajima alisema kumekuwa na uvumi
kwamba kuhojiwa kwake na polisi kulitokana na kuwakaribisha wanasiasa
hao kanisani kwake kwa nyakati tofauti na kuzungumza na waumini wake.
Alisema alifahamiana na Lowassa tangu mwaka 1996
wakati huo mbunge huyo akiwa Waziri wa Ardhi na tangu kipindi hicho
amekuwa mtu wake wa karibu.
Alisema alifahamiana na Dk Slaa tangu mwaka 1994
kabla hajagombea nafasi ya urais kupitia Chadema na kwamba tangu wakati
huo amekuwa rafiki wa familia.
“Hawawezi kunichagulia marafiki, hawa ni watu
wangu wa karibu hata kabla hawajawa na ndoto za kugombea urais,
nitaendelea kuwa nao karibu,” alisema.
Asimulia mahojiano
Akizungumzia mahojiano yake na polisi, Gwajima
aliwaeleza waumini wake kwamba mambo mengi aliyohojiwa hayakuhusiana na
suala la kumkashifu Kardinali Pengo.
“Polisi walinihoji mambo mengi binafsi
yanayonihusu mimi na hayakuhusiana kabisa na Pengo, maswali ya Pengo
yalikuwa machache sana,” alisema.
Hata hivyo, Gwajima alisema hana ugomvi na polisi
wala Serikali kwa kuwa amekuwa akitoa ushirikiano kwa vyombo hivyo.
Akitoa mfano, alisema Februari mwaka huu alipeleka barua polisi kueleza
anataka kudhamini kampeni kwa ajili ya kupinga mauaji ya albino kwa
kushirikiana na jeshi hilo.
“Niliwaeleza kwamba tungezunguka na polisi mikoa
yote Tanzania na wamenijibu kwamba nipeleke ratiba ya shughuli hiyo ili
tuanze,” alisema.
Alisema pia alidhamini mafunzo ya ulinzi
shirikishi kwa vijana 400 kwa kushirikiana na polisi... “Shughuli hizi
zinaonyesha kwamba sina ugomvi na polisi, bali nimekuwa rafiki kwa
kushiriki katika shughuli zenye masilahi kwa Taifa.”
Viongozi wamiminika
Alisema pia hana ugomvi na Serikali na kwamba viongozi wake wamekuwa wakimiminika katika kanisa lake.
Aliwataja viongozi hao kuwa ni Waziri Mkuu
mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Waziri wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe.
Viongozi wengine, alisema ni Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa CCM, Nape Nauye, Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee na
wabunge wa Viti Maalumu, Dk Mary Mwanjelwa na Vicky Kamata wote wa CCM
“Kama ningekuwa na ugomvi na Serikali viongozi hawa wasingekuja katika kanisa langu kwa nyakati tofauti. Hii inaonyesha nilivyo na uhusiano mzuri na Serikali,” alisema.
“Kama ningekuwa na ugomvi na Serikali viongozi hawa wasingekuja katika kanisa langu kwa nyakati tofauti. Hii inaonyesha nilivyo na uhusiano mzuri na Serikali,” alisema.
Alhamisi ijayo
Askofu Gwajima amewataka waumini wake kumsindikiza
katika Kituo cha Polisi siku ambayo atahojiwa kwa mara nyingine.
“Nitakwenda Central Police Alhamisi saa moja asubuhi, nawaomba waumini
wote mfike katika eneo hilo lakini msilete fujo wala kumtukana mtu,
kuweni watulivu wakati wote nitakapokuwa nahojiwa,” alisema.
Askofu huyo alitakiwa kuhojiwa Alhamisi iliyopita lakini polisi waliahirisha kutokana na hali yake kutokuwa ya kuridhisha.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar
es Salaam, Suleiman Kova alisema Jeshi la Polisi halitaruhusu
mkusanyiko wa watu katika eneo hilo wakati Askofu Gwajima atakapohojiwa.
“Atatakiwa kufika na wakili wake na mtu mmoja
ambaye ataona anafaa kuingia naye kwenye mahojiano. Kama kuna waumini
wanajiandaa kukusanyika katika ofisi zetu hapa Central Polisi, wafahamu
kwamba haturuhusu na wakikaidi tutachukua hatua.”
Ilivyokuwa kanisani
Gwajima alifika katika kanisa hilo lililopo kwenye
viwanja vya Tanganyika Packers Kawe saa 5.00 asubuhi na kupokewa kwa
shangwe na waumini walioanza kufika tangu saa 2.00 asubuhi.
Msafara wa magari matatu; Toyota Land Cruiser
mbili na Hammer, yaliwasili kwenye viwanja vya kanisa hilo na kulakiwa
na waumini walioyazingira kwa shangwe na vigelegele wakitaka kumwona
Askofu Gwajima.
Waumini hao walikuwa na shauku ya kumwona Gwajima na walionekana wakisukumana ovyo kila mmoja akitaka kumwona.
Akiwa amevaa suti ya rangi ya kijivu na shati
jekundu, Gwajima aliteremka katika Hammer akishikiliwa na wasaidizi wake
na kukalishwa katika kiti cha magurudumu mawili kilichokuwa kikisukumwa
na wasaidizi hao kuelekea kwenye jukwaa la kanisa hilo.
Baada ya kufika, vikundi vya kwaya viliendelea kuimba na kucheza nyimbo mbalimbali za kumtukuza Mungu.
Gwajima alizungumza na waumini wake kuanzia saa
5.30 hadi saa 6.45, akiwaeleza kilichotokea kuanzia siku alipofika
polisi kwa mara kwanza, mahojiano hadi alipotoka hospitali.
Katika mahubiri yake, Gwajima alisema ataendelea
kuwaonya viongozi wa Serikali na wa dini watakaokosea masuala
mbalimbali.
“Sitajali ni kiongozi wa aina gani amekosea nitawakemea. Rais akikosea nitamkemea. Waziri akikosea nitamkemea na viongozi wa dini wakikosea nitaendelea kuwakemea,” alisema.
“Sitajali ni kiongozi wa aina gani amekosea nitawakemea. Rais akikosea nitamkemea. Waziri akikosea nitamkemea na viongozi wa dini wakikosea nitaendelea kuwakemea,” alisema.
Post a Comment