Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat
Gwajima amemwomba Rais Jakaya Kikwete kuvikemea vyombo vya dola
vinavyomfuatafuata vikihoji mambo binafsi na kwamba akishindwa kufanya
hivyo itakuwa wazi kwamba yeye ndiye anawatuma.
Akihubiri mamia ya waumini wa kanisa hilo jana,
Gwajima alisema amekuwa akifuatwafuatwa na vyombo vya Serikali utadhani
yeye si raia wakati ni Mtanzania halisi.
“Rais Kikwete tafadhali namuomba awakemee watu
hawa... asipowakemea, basi kanisa langu litajua kwamba yeye ndiye
anayewatuma,” alisema Gwajima huku akishangiliwa na waumini waliokuwa
wakimsikiliza.
Huku wakinyeshewa na mvua, waumini hao walikuwa
wakimsikiliza Askofu Gwajima, siku tatu baada ya kiongozi huyo kuhojiwa
kwa mara ya pili na polisi na kutakiwa awasilishe mambo 10 yanayohusiana
na usajili wa kanisa, uongozi na mali zake.
Uraia wake
“Mimi ni Mtanzania halisi acheni nifanye kazi ya
Mungu, kama mnadhani mimi si Mtanzania, basi mmepotoka kwani kwa hilo
mtashindwa,” alisema.
Alisema makundi ya jamii yamekuwa yakitoa kauli mbalimbali lakini hayabughudhiwi anavyofanyiwa.
“Madaktari, wanasiasa, wafanyabiashara wamekuwa
wakitoa misimamo yao lakini hawabughudhiwi iweje Gwajima tu? Nitaendelea
kuwapa vidonge vyenu kila mtakapopotoka, nafanya kazi ya bwana,”
alisema.
Kuhusu utajiri wake
Gwajima alisema amekuwa akishangazwa na vyombo vya
Serikali vinavyohoji utajiri alionao bila kujua anaongoza idadi gani ya
waumini. Alisema anaongoza kanisa lenye waumini zaidi ya 70,000 ambao
ni kama watoto wake na kwamba yeye ni baba yao wa kiroho.
“Waumini hawa mimi ni baba yao wa kiroho,
nikiwaomba kila mmoja anipe Sh1,000 tu nitakuwa na Sh70 milioni, halafu
mnahoji utajiri ninaupata wapi?” alisema na kisha kuwauliza waumini
hao... “Hivi baba yenu nikiwaomba kila mmoja anipe Sh1,000 mtanipa au
mtaninyima?”
Alijibiwa, “Tutakupaaaa!” Baada ya majibu hayo
waumini hao walianza kupeleka fedha katika jukwaa kuu huku wakiimba
nyimbo za kumtukuza Mungu.
Post a Comment