Hannival akipapasa zeze la Kihabeshi
Timu kamili ya Ethio-Swahili Fusion wakishambulia
Shabiki kutoka Brazil akimpongeza Dr Mulatu
Leo Mkanyia akimkaribisha rasmi King of Ethio Jazz Dr Mulatu
Dr Mulatu na Leo wakishambulia jukwaa
Wadada wa Kihabeshi wakitwanga Swahili Blues kihabeshi habeshi
Dr Mulatu na Leo wakishambulia jukwaa
Mkongwe Dr Mulatu akimtoa kamasi Leo
Siku ya Jumamosi ya tarehe 4 April 2015 mjini Addis Ababa, historia
iliandikwa pale Leo Mkanyia na Swahili Blues Band walipopiga jukwaa
moja na gwiji la muziki la kimataifa na mfalme wa Ethio Jazz Dr Mulatu
Astatke katika ukumbi maarufu wa African Jazz Village.
Shoo hiyo kali sana na ya kihistoria ilianza saa tatu kamili za jioni
pale Swahili Blues Band walipofanya ufunguzi kwa kupiga nyimbo zao kwa
takriban saa moja kabla ya kumkaribisha Dr Mulatu ukumbini. Nyimbo hizo
zilizokuwa na mahadhi kamili ya Kitanzania ziliwabamba vilivyo wapenzi
lukuki waliohudhuria na kubahatika kuwa miongoni mwa watu walioshuhudia
historia ikitengenezwa. Wapenzi hao wa mataifa mbali mbali walibambika
vilivyo na miziki hiyo iliyoundwa kutoka makabila mbalimbali ya
Kitanzania yakiwemo ya Kimakua, Kizaramo, Kingoni na Kimakonde.
Utamaduni halisi wa Kitanzania ulidhihirishwa pale wanamuziki
walipocheza mirindimo ya ngoma kama vile Mtara ya kimakua, mdundiko,
lizombe na sindimba.
Muziki huo wa Kitanzania ulihudhuriwa na wageni wengi wakiwemo wageni
maalumu kama vile mabalozi kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Brazil,
Argentina, Ufaransa, Lebanon, Israel, Marekani na wawakilishi kutoka
mashirika kama vile UNHCR, UNICEF na Alliance Francaise.
Nyimbo za ufunguzi zilizopigwa na Swahili Blues Band zilikuwa pamoja na Dunia Hii, Mwanangu, Mdundiko, Binti Ally na Che Maria.
Saa nne kamili Leo Mkanyia alimkaribisha rasmi jukwaani Dr Mulatu kwa
ajili ya kujiunga rasmi kupiga pamoja na Swahili Blues Band. Dr Mulatu
alikuja na mwanamuziki mmoja kutoka Ethiopia anayepiga zeze la kiasili
la ki Ethiopia pamoja na wanenguaji wawili wa kike wanaocheza mirindimo
ya ki Ethiopia. Dr Mulatu alipiga vingoma vyake vidogo viwili pamoja na
chombo chake mahsusi ambacho ni marimba ya umeme yaani Xylophone huku
akitegemea mirindimo kutoka nyimbo za Swahili Blues.
Dhana nzima ya shoo hii ilikuwa ni kukutanisha tamaduni kutoka Afrika
Mashariki na Ethiopia.Ilikuwa fursa mahsusi yakukutanisha Swahili Blues
na Ethio Jazz.Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa gwiji huyu kupiga
jukwaa moja na kwa pamoja na wanamuziki kutoka Afrika Mashariki huku
gwiji akipiga muziki wa Kitanzania. Kwa mujibu wa Dr Mulatu, mirindimo
hii ya Kitanzania inashabihiana sana na ngoma kutoka kaskazini mwa
Ethiopia. Na hii ndiyo ilirahisisha kwake kufanya fusion hii mahsusi na
maalumu kabisa.
Nyimbo sita za Swahili Blues zilipigwa kwa umahiri wa hali ya juu huku
Dr Mulatu akijibishana kwenye ngoma na mpiga ngoma maarufu wa Swahili
Blues Bwana Juma Setumbi. Mabishano hayo yaliendelea tena pale Juma
alipohamia kwenye marimba ya kiswahili na mkongwe kuhamia kwenye
Xylophone yake.Yalikuwa ni majibishano yaliyonoga kwa sana kabisa. Mamia
ya wapenzi waliripuka kwa shangwe, nderemo, mbinja na vifijo pale
majibishano hayo yalipokuwa yakiendelea. Kwa kweli ilikuwa ni shoo
kabambe na ya kimataifa.
Nyimbo zilizopigwa katika fusion hiyo zilikuwa ni Seychelles, Afrika, Aichelelo, Wazazi Wangu, Sawa Saware na Bwana Mdogo.
Baadhi ya wapenzi waliohudhuria walihojiwa na waandishi wetu na kutoa maoni mbalimbali juu ya shoo hii kama ifuatavyo;
-Solomon Alemayehu kutoka Ethiopia- hii ni shoo kabambe ambaye haijawahi
kutokea hapa Ethiopia kwenye miaka ya karibuni. Hakika hii bendi ni
kali kweli kweli na miziki yake ni kitamaduni haswaa. Sijawahi kuona Dr
Mulatu akipiga huku akitoka jasho namna ile.Hakika historia imeandikwa
leo.
- Muna Tadese, Mmarekani mwenye asili ya ki Ethiopia anayeishi Atlanta
Marekani- maingiliano ya kiutamaduni tuliyoyaona leo hakika
yamedhihirisha kuwa Afrika ni nchi moja kubwa kiutamaduni. Kazi nzuri
sana imefanyika jioni ya leo.
-Luiza Benicio kutoka Salvador Brazil- shoo ya leo imenikumbusha ngoma
na dansi maalumu inayopigwa nchini kwetu maarufu kama Capoeira.
Nitafanya juhudi kubwa kuhakikisha Bendi hii inakuja nchini Brazil
kuendeleza mahusiano mazuri ya kiutamaduni miongoni mwetu.
Nimefurahishwa sana
Post a Comment