KUNA UMUHIMU WA KUMFUATILIA, KUMCHUNGUZA MPENZI WAKO?

UHALI gani mpenzi msomaji wa safu yetu ya Show the Love. Bila shaka uko vizuri na kama pia ni mgonjwa, nakuombea kwa Mungu akutie nguvu upone haraka.Tukilifungua jamvi letu la leo, kama linavyojinasibu hapo juu katika kichwa cha habari. Mapenzi ni hisia, kuna tafsiri ambayo inasema mtu asipokufuatilia, asipokuchunguza katika mapenzi basi hakupendi. Watu utawasikia wakisema, lazima umfuatilie mpenzi wako ili ujue nyendo zake vinginevyo utaibiwa maana dunia ya sasa suala la watu kuibiana wapenzi limekithiri.
Wapo wanaosema licha ya kumfuatilia nyendo zake, lazima umchunguze vitu. Bila yeye mwenyewe kujua, unatumia mbinu zako za kumhoji maswali, kumsachi simu yake au kuangalia pochi yake ameweka vitu gani.
Wengine humchunguza mwenzake ananukiaje, kama akigundua kuna harufu nyingine ananukia tofauti na aliyoizoea, tayari anaanza kutia shaka na kuzidisha uchunguzi kwa mhusika.
Tafsiri hiyo inaweza kuwa na namna mbili. Kukufuatilia au kumchunguza mtu kwa kiasi fulani huwa ni jambo jema lakini unafanya hayo mkiwa katika hatua gani na unafanya kwa kiasi gani maana ukizidisha kumfuatilia mwenzako, haitakuwa mapenzi tena, itakuwa ni kero.
Kuna msomaji mmoja alinitumia ujumbe mfupi wa maandishi akitaka nimshauri. Acha niuandike hapa kwa faida ya wengine ambao wanasumbuliwa na tatizo hili:“Anko naomba unisaidie, nina mchumba wangu nampenda na yeye ananipenda. Tumedumu naye katika uhusiano kwa zaidi ya miaka minne lakini tatizo lake ananifuatilia sana. Ananichunguza kila hatua ninayopiga hadi imekuwa kero.
“Ameniwekea watu wa kunifuatilia kila kona eti wampe taarifa zangu, na ukikutana naye maswali hayaishi, sijui kwa nini haniamini, wakati sina mtu zaidi yake, naomba ushauri wako.”Nikimjibu msomaji huyo, naamini wote tutajifunza kwa pamoja. Kumchunguza mtu ni jambo jema lakini jambo hilo linapaswa kufanyika mapema kabla hujaamua kumkabidhi mwenzako moyo wako.
Kabla ya kuanzisha uhusiano jiulize, ni mtu wa aina gani na mwenye sifa zipi anafaa kuwa mpenzi wako. Usiwe na papara, chukua muda mrefu kumchunguza usije kujikuta umeangukia kwenye mikono isiyo salama.
Akijitokeza mwenye sifa unazozihitaji basi huo ndiyo wakati mzuri wa kuanza kumchunguza mwenzako. Mchunguze tabia zake, mweke karibu ili uweze kumjua vizuri nyendo zake na uweze kufanya uamuzi sahihi.
Mfanye awe rafiki ili uweze kuwajua wanaomzunguka. Wakati mwingine mtu unamjua kwamba ni wa aina gani pindi unapokuwa naye karibu. Mfanye awe rafiki wa karibu kabla hajawa mpenzi wako.Mfuatilie njia zake maana tabia ya mtu haijifichi hata siku moja. Anaweza akaficha makucha yake kwa kipindi fulani lakini haiwezi kuwa moja kwa moja, kuna siku atakunjua makucha yake na utakuwa umeshamjua tabia zake.
Zipime hizo tabia zake kama ni za kawaida na je, zinaweza kurekebishika? Kama tabia mbaya za kiasi, waweza kumshauri huku ukifuatilia mabadiliko yake.Ukifika wakati umeona mnakwenda katika mstari ulionyooka, anzisheni uhusiano mzito wa mapenzi ambao una malengo mazuri. Usikubali kuanzisha uhusiano na mtu ambaye hujajiridhisha kama ana sifa nzuri kitabia.
Ingia kwenye uhusiano na mtu unayemuamini anafaa. Ana mawazo chanya, unayeamini hata kusumbua mbeleni.Hakuna haja ya kumfuatilia mwenzako kupita kiasi. Unachotakiwa ni kumjengea mazingira ya kuwa na imani naye. Mjengee mazingira ya kumuheshimu naye atakuheshimu.
Mpenzi wako huwezi kumchunga hata iweje. Kuna wakati utahitaji uende kazini, utakuwa mbali naye kwa namna yoyote. ukishamuwekea mazingira ya kuheshimiana, kamwe hawezi kukuvunjia heshima.
Hakuna umuhimu wowote wa kumuwekea watu wa kumfuatilia mchumba wako. Kwanza ni udhaifu halafu pia wanaweza wakakupa taarifa ambazo si za kweli. Yule unayemfuatilia, akigundua kwamba unamfuatilia, atajisikia vibaya, ataona humuamini.
Hakuna kitu kibaya kama mtu kuishi katika uhusiano huku ukijua kuwa mwenziyo hakuamini. Hawezi kuwa na amani juu ya chochote anachokifanya. Matokeo yake naye atapoteza imani na wewe.

Post a Comment

Previous Post Next Post