MAUAJI YA POLISI 2 MKOA WA PWANI UGAIDI UGAIDI


HUKU watu wakisherehekea Sikukuu ya Pasaka kwa vifijo, shangwe na nderemo, kwa familia za polisi waliouawa Vikindu wilayani Mkuranga, Pwani,  Sajenti Michael Aaron Tuheri (49) na Koplo Francis Mkinga (53) ilikuwa ni huzuni kutokana na vifo vya wapendwa wao hao.
Mauaji ya polisi hayo yamewaacha ndugu na jeshi la polisi nchini katika hali ya huzuni huku yakifananishwa na yale yaliyotokea katika vituo mbalimbali vya polisi nchini yanayofananishwa na ugaidi.Tukio hilo lililotokea saa 1:30 usiku wa Machi 30, mwaka huu katika kizuizi cha barabarani kilichopo Kijiji cha Kipara, Kata ya Vikindu ni mfululizo wa utekaji wa askari na vituo vya polisi katika Mkoa wa Pwani.
Juni 11, 2014, watu wenye silaha za jadi walivamia Kituo cha Polisi cha Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga mkoani humo na kumuua kwa kumshambulia kwa mapanga Askari Joseph Ngonyani kisha kupora bunduki tatu aina ya SMG na risasi 50.
Januari 21, mwaka huu, watu wasiojulikana walivamia Kituo cha Polisi cha Ikwiriri, Rufiji mkoani humohumo na kuwaua askari wawili, Koplo Edgar na WP Judith na kupora silaha zilizokuwepo kituoni hapo.Katika tukio hilo la Vikindu, polisi hao walikuwa wanne ambapo wawili walikuwa wanakula huku wengine wakiwa barabarani.
Mara baada ya tukio hilo, timu ya waandishi wa habari za uchunguzi wa Gazeti la Uwazi ilitinga katika eneo hilo na kufanya mahojiano na wakazi wake ambao walikuwa na haya ya kusema:
“Mimi nilikuwa ninapita pale niliwaona watu kama kumi hivi wakielekea katika kizuizi walipokuwa polisi. Baada ya muda mfupi nilisikia kelele za mtu akilia, akisema ‘msiniue mnanikata, nimewakosea nini?’ Halafu ghafla nikasikia milio ya risasi, nilijua kuna uvamizi.
Miili ya polisi hao ikiagwa.
“Mimi na baadhi ya majirani tuliulizana lakini bila kupata majibu. Baadaye ndipo tukapata habari kwamba polisi wawili wameuawa na majambazi na mmoja wao (Sajenti Ali) amejeruhiwa.“Polisi hawakuchukua muda mrefu kufika lakini walikuta wahalifu hao wameshaishia zao.“Hawa watu ni wabaya sana, hivyo IGP Ernest Mangu asipochukua hatua haraka polisi watakuwa wanauawa na kunyang’anywa silaha kila kukicha.”
“Mimi naamini hawa watu wanakusanya silaha, naamini kuna jambo kubwa watalifanya huko mbele maana hata Boko Haramu walianza kidogokidogo na kwa sasa wanaisumbua serikali ya Nigeria.“Kuna haja ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) kushirikiana na polisi kukomesha hii hali, hatuna raha kuona vijana wetu wanatekwa na kuuawa kinyama kila kukicha bila hata hatua madhubuti kuchukuliwa. Huu ni ugaidi, ugaidi kwa sababu haiwezekani jambazi avamie, waue na kuchukua silaha za kivita.”Mkuu wa Mkoa wa Dara es salaam Meck Sadick akiaga mwili wa marehemu.
Vyanzo vyetu makini ndani ya jeshi la polisi vinadai kwamba wakati polisi hao wanavamiwa, Francis alishtukia kitu chenye makali kikiingia shingoni, aliishiwa nguvu, bunduki ikadondoka na kuchukuliwa na mmoja wa watu hao.
Michael yeye alipigwa risasi ya mgongoni na kutokea kifuani, wote wakafariki dunia papo hapo, wakati huo sajenti Ali alikimbia na bunduki iliyobakia huku akijeruhiwa na risasi mguuni.Taarifa toka kwa marafiki wa marehemu Francis zinadai kwamba, ni kama walijua watakufa kwani aliwahi kusema kuwa kwenye kizuizi wanapangwa wachache wakati kizuizi hicho kipo porini hivyo kuna siku wanaweza kuvamiwa kirahisi.
Baadhi ya maafisa wa jeshi la polisi wakiwa wamebeba jeneza.
Agnes Michael, mke wa marehemu Michael alipohojiwa na Uwazi juu ya kifo cha mumewe alisema:
“Ilikuwa saa 2:30 usiku wa kuamkia Jumanne ndipo nilipopata taarifa kutoka kwa afande mwenzake kwamba mume wangu ameuawa na watu wasiojulikana akiwa kazini.Nilipata mshtuko mkubwa sana kwani tulikuwa tukiishi vizuri. Ni mwaka juzi tu tulifunga ndoa,” machozi yakamtoka.
Moja ya jeneza likipakiwa kwenye gari.
IGP MANGU NAYE
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu (pichani) aliwataka askari kujipanga kwa sababu wanapambana na watu wanaotaka kuwapunguza nguvu za polisi.“Tutumie msiba huu kuhakikisha hawa watu tunawashinda. Pia tunawaomba wananchi watupe ushirikiano.” alisema Mangu.

Post a Comment

Previous Post Next Post